IQNA

Singapore yapiga marufuku kitabu kilicho dhidi ya Uislamu

13:47 - November 02, 2021
Habari ID: 3474506
TEHRAN (IQNA)- Serikali ya Singapore imetangaza kupiga marufuku kitabu ambacho kina taswira zinazomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Kwa mujibu wa idara inayosimamia vyombo vya habari Singapore, IMDA, Kitabu hicho chenye anuani ya “Red Lines: Political Cartoons and the Struggle Against Censorship,” kimebainika kuwa na taswira zenye kuvunjia heshima dini zikiwemo zile zilizochapishwa Ufaransa na jarida la Charlie Hebdo zenye kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Taarifa hiyo imesema: "Katuni zisizo za heshima za Charlie Hebdo zilichapishwa kwa mwa ya kwanza mwaka 2006 na zimetajwa kuwa zisizo za uwajibikaji za kijeuri na za kibaguzi."

IMDA imesema kitabu hicho pia kilikuwa na taarifa zenye kuvunjia heshima dini za Kikristo na Kihindu na kwa msingi huo kimepigwa marufuku. Yeyote atakayepatikana akiagiza kutoka nje ya nchi, kuuza, kusambaza au kuchapisha kitabu hicho atatozwa faini ya hadi dola 3,700 au kufungwa kwa mwaka moja jela au yote mawili.

Singapore au Singapuri ni nchi ndogo na iliyostawi katika Asia ya Kusini-Mashariki ambayo uchumi wake unategemea zaidi biashara, hasa benki pamoja na viwanda. Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia 15 ya watu wote milioni 5.6 katika nchi hiyo.

Singapore ina sheria kali za kuzuia matamshi au maandishi ya chuki na vitendo vyote ambavyo vinaweza kuibua uhasama baina ya wafuasi wa dini mbali mbali nchini humo.

/4009919

captcha