IQNA

Waislamu Singapore

Idadi ya Wasingapuri wanaokwenda Umrah yaongezeka

16:19 - March 02, 2023
Habari ID: 3476647
TEHRAN (IQNA) – Idadi ya Waislamu kutoka Singapore wanaofanya ibada ya Hija ndogo ya Umrah imeongezeka kwa asilimia 45 ikilinganishwa na enzi ya kabla ya janga la corona.

Hayo yametangazwa na Waziri wa Hija na Umrah wa Saudia Tawfiq Al-Rabiah alipofanya ziara katika nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia.

Rais wa Singapore Halimah Yacob amempokea waziri huyo wa Saudia siku ya Jumatano kama sehemu ya ziara yake rasmi pamoja na ujumbe wa wawakilishi kadhaa kutoka serikali na taasisi za kibinafsi zinazohusika na kuwahudumia watu wa Singapore wanaoshiriki katika  Hija na Umrah.

Wakati wa mkutano huo, Al-Rabiah alitaja kuwa msimu wa Hija wa mwaka huu utaona kurudi kwa Mahujaji katika viwango vyao vya kabla ya janga la corona.

Pia aliangazia kuongezeka kwa idadi ya Wasingapuri wanaoshiriki ibada ya Umrah  kwa 45% ikilinganishwa na viwango vya kabla ya janga la corona na kusema hilo linatokana na kuimarika ubora wa huduma.

Katika ziara hiyo, pande hizo mbili zilijadili njia za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati baina ya nchi hizo mbili ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa watu wa Singapore wanaoelekea Saudia kwa ziara za kidini.

Singapore au Singapuri ni nchi ndogo na iliyostawi katika Asia ya Kusini-Mashariki ambayo uchumi wake unategemea zaidi biashara, hasa benki pamoja na viwanda. Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia 15 ya watu wote milioni 5.6 katika nchi hiyo.

Singapore ina sheria kali za kuzuia matamshi au maandishi ya chuki na vitendo vyote ambavyo vinaweza kuibua uhasama baina ya wafuasi wa dini mbali mbali nchini humo.

3482677

captcha