IQNA

Waislamu Singapore wahakikishiwa usalama kufuatia njama ya kuhujumu misikiti

16:45 - January 30, 2021
Habari ID: 3473606
TEHRAN (IQNA)- Waislamu nchini Singapore wamehakikishiwa usalama wao baada ya kubainika kuwepo njama ya kushambulia misikiti nchini humo.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiislamu la Singapore (Muis) Esa Masood amewataka Waislamu kutulia huku akiwahimiza viongozi wa misikiti kushirikiana na taasisi zingine kwa ajili ya usalama misikitini. Amesema watahakikisha kuwa misikiti inaendelea kuwa eneo salama kwa ajili ya waumini wote wakiwemo watoto. Tamko hilo limekuja baada ya kubainika kuwa kijana mmoja wa kanisa la Protestanti mwenye asilia ya India alikuwa analenga kuwashambulia Waislamu katika misikiti miwili ya Masjid Yusof Ishak huko Woodlands Masjid Assyafaah eneo la Sembawang.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Singapore K. Shanmugam amesema maeneo ya ibada hayapaswi kubadilishwa kuwa vituo vya kijeshi. Ametoa wito kwa jamii kuhakikisha zinatoa mafunzo kwa vijana ili wajiepushe na misimamo mikali.

Imedokezwa kuwa kijana huyo Mkristo mwenye umri wa miaka 16 alikuwa analenga kutekeleza mashambulizi kama yale yaliyotekelezwa na gaidi mmoja  Mkristo nchini New Zealand katika mji wa Christchurch ambapo aliwaua Waislamu 51 katika hujuma dhidi ya misikiti miwili wakati wa Sala ya Ijumaa.

Singapore au Singapuri ni nchi ndogo na iliyostawi katika Asia ya Kusini-Mashariki ambayo uchumi wake unategemea zaidi biashara, hasa benki pamoja na viwanda. Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia 15 ya watu wote milioni 5.6.

3473839

captcha