IQNA

Umoja wa Afrika wabatilisha uamuzi wa Israel kuwa mwanachama mwangalizi

17:06 - February 07, 2022
Habari ID: 3474901
TEHRAN (IQNA)- Umoja wa Afrika (AU) umesimamisha nafasi ya mwanachama mwangalizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika umoja huo hatua ambayo ni pigo kwa utawala huo unaokaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.

Taarifa kutoka kwenye mkutano wa 35 wa siku mbili wa  viongozi wa Umoja wa Afrika (AU)  uliomalizika Jumapili huko Addis Ababa zinasema kuwa umoja huo umefuta uamauzi wa awali wa kuupa utawala haramu wa Israel hadi ya  mwanachama mwangalizi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni wa Israel Januari 22 mwaka huu ilitangaza kuwa Aleligne Admasu, balozi wa utawala huo nchini Ethiopia, amekabidhi hati yake ya utambulisho kama mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika.

Vyombo vya habari vya Kiarabu vimeripoti kuwa, nchi saba za Kiarabu zilitangaza wazi kupinga uamuzi wa AU wa kuupatia utawala wa Kizayuni hadhi na nafasi ya mwanachama mwangalizi ndani ya Umoja wa Afrika; suala ambalo pia limeungwa mkono na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Huko nyuma utawala wa Kizayuni wa Israel uliwahi kupewa nafasi ya mwangalizi ndani Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) lakini baada ya kuvunjika umoja huo mwaka 2002 na kubadilishwa kuwa Umoja wa Afrika (AU) jitihada za utawala wa Kizayuni za kuendelea kupewa nafasi hiyo ziligonga mwamba. 

Ramtane Lamamra Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria  jana aliiambia televisheni ya France 24 akiwa Addis Ababa, kuwa hatua ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika ilikuwa uamuzi mbaya wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ambao ulichukuliwa bila ya kushauriana na wanachama wa umoja huo.  

Afrika Kusini na Algeria zimekuwa mstari wa mbele kupinga  utawala wa kibaguzi wa Israel kuwa mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika. Kwa muda mrefu Umoja wa Afrika umekuwa mstari wa mbele kutetea Wapalestina ambao ardhi zao zinakoloniwa na utawala wa kibaguzi wa Israel.

4034317

captcha