IQNA

Jeshi la IRGC la Iran latangaza kulenga kwa makombora kituo cha Wazayuni

20:37 - March 13, 2022
Habari ID: 3475035
TEHRAN (IQNA)- Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) limetangaza kuwa limelenga kwa makombora kituo cha kistratijia cha njama na uovu cha Wazayuni na kusisitizia kuwa: Kurudiwa kwa uovu wa aina yoyote kutakabiliwa na jibu kali, la pande zotei na haribifu.

Asubuhi ya leo (Jumapili) vituo viwili vya kijasusi vya Shirika la Ujasusi na Operesheni Maalumu la utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) mjini Erbil, huko Kaskazini mwa Iraq, vimepigwa kwa makombora yaliyorushwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran.

Kufuatia operesheni hiyo kubwa ya makombora na maroketi, kulisikika sauti za ving'ora na kengela ya hatari katika ubalozi mdogo wa Marekani huko Erbil, eneo la Kurdistan ya Iraq; na kambi zote za kijeshi za Marekani nchini Iraq zimewekwa katika hali ya tahadhari.

Taarifa ya Idara ya Uhusiano wa Umma wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imesema: Kufuatia jinai za hivi karibuni za utawala bandia wa Israel, na tangazo la hapo awali na IRGC la kutonyamazia kimya jinai za utawala huo, jana usiku, "kituo cha kistratijia cha njama na uovu wa Wazayuni" kililengwa kwa makombora erevu ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Taarifa hiyo imeliambia taifa la Iran kwamba: "Usalama na amani ya ardhi ya Kiislamu ni mstari mwekundu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ,na hakuna upande wowote atakaoruhusiwa kuitishia au kuishambulia."

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, mapema leo ripoti za vyombo vya habari vya Iraq na duru za kijeshi za nchi hiyo zimeeleza kuwa, kambi mbili za kutoa mafunzo za Shirika la Ujasusi la Israel (MOSSAD) zimeshambuliwa kwa makombora ya balestiki katika eneo la Erbil, Kaskazini mwa Iraq.

Duru za kiintelijensia za eneo la Kurdistan zinaarifu kuwa, makombora 12 ya balestiki yametumika katika shambulio hilo la alfajiri ya leo katika mji wa Erbil. 

4042623

captcha