IQNA

17:18 - May 12, 2022
Habari ID: 3475241
TEHRAN (IQNA)- Ufaransa imemtimua kutoka nchi hiyo mhubiri mmoja wa Kiislamu Mkomoro na familia yake baada ya kusikika akisoma aya za Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume SAW zinazowahimiza wanawake Waislamu wajisitiri, wakae nyumbani na wawatii waume zao.

Sheikh Ahamada Mmadi, 35 ambaye alikuwa Imamu wa Msikiti wa Saint-Chamond, ametimuliwa Ufaransa na kurejeshwa Visiwa vya Komoro kwa sababu ya kile ambacho kimetajwa na wakuu wa serikali kuwa  ni 'matamshi yanayokinzana na misingi na sheria za Jamhuri."

Sheikh Mmadi amechukuliwa hatua baada ya kunukulu sehemu ya aya ya 33 ya Surah Al Ahzab ambapo Allah SWT anawahutubu wanawake kwa kusema: " Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani..."

Aidha katika hotuba yake, Sheikh Mmadi alinukulu hadithi ya Mtume SAW kuwa, iwapo mwanamke atasali sala tano nyumbani, afunge Mwezi wa Ramadhani, alinde staha yake, na amtii mume wake, basi ataingia peponi kwa mlango wowote ule atakao.

Hatahivyo wakuu wa Ufaransa katika eneo la Loire wamedai kuwa hotuba hiyo ambayo ilitolewa wakati wa Sala ya Idul Fitr mwaka huu ilikuwa ya 'kibaguzi' na hivyo Sheikh Mmadi ametimuliwa nchini humo.

Mwezi Julai mwaka jana pia alisimamishwa kwa muda kazi zake kama imamu wa msikiti kufuatia ombi la maafisa wa serikali ya mtaa kwa kutoa hotuba nyingine ambayo ilitajwa kuwa ya kibaguzi na inayokinzana na usawa wa mwanamke na mwanaume.

Baada ya kutangazwa amri ya kumtimua, Sheikh Mmadi amesema: "Sijuti chochote. Haya si maneno yangu, ni maneneo ya Allah SWT na Mtume Wake. Kile ambacho nimefanya ni kukariri yalivyo katika vitabu vitakatifu."

Mwaka uliopita,  Bunge la Kitaifa la Ufaransa liliidhinisha sheria ya 'Thamani za Jamhuri' ambazo zilipendekezwa na rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'

Jumuiya ya Waislamu Ufaransa (CFCM) imepinga vikali sheria hiyo na kuitaja kuwa yenye kuwawekea Waislamu vizingiti katika maisha yao yote.

Sheria hiyo inaipa serikali haki ya kuingilia mambo ya misikiti kama vile hotuba na kupeleleleza kamati zinazosimamia misikiti na pia kudhibiti matumizi ya pesa za misikiti na asasi za Waislamu.

3478857

Kishikizo: Ahamada Mmadi ، ahazab ، ufaransa
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: