IQNA

Maandamano Ufaransa kupinga kushadidi chuki dhidi ya Uislamu

23:07 - February 15, 2021
Habari ID: 3473652
TEHRAN (IQNA)- Mwenedo wa chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya hususan nchini Ufaransa ungali unaendelea ambapo Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakikabiliwa na mashinikizo makubwa.

Hali hiyo imepelekea akthari ya wananchi wa Ufaransa wakusanyike katika mji mkuu wa nchi hiyo Paris na kuandamana wakipinga mpango wa serikali ambao unalenga kushadidisha mibinyo na mashinikizo dhidi ya Waslamu wa nchi hiyo.

Serikali ya Ufaransa inakusudia kupasisha mpango ambao kwa mujibu wake baadhi ya uhuru wa kidini katika nchi hiyo ya bara Ulaya utawekewa mipaka na kimsingi akthari ya Waislamu ndio watakaokuwa washukiwa wakuu.

Katika miezi ya hivi karibuni wimbi la chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa limeshadidi ambapo Waislamu wengi wamekuwa waiandamwa kwa mashinikizo na vitendo vya bughuda ha na mauadhi na hata wakati mwingine matukufu ya dini yao kutusiwa na kuvunjiwa heshima.

Rais Macron atetea chuki dhidi ya Uislamu

Hii ni katika hali ambayo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa naye katika misimamo yake siyo tu kwamba, hajayachukulia hatua makundi yanayoendesha vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu, bali ameyatetea na kuyakingia kifua kwa jina la uhuru wa kujieleza.

Katika uwanja huo, serikali ya Paris imewasili muswada wa “Sheria ya Kuimarisha Thamani za Kijamhuri” ikidai kwamba, muswada huu haukinzani na dini nyingine na lengo lake hasa ni kutetea uhuru. Rais wa Ufaransa katika kutetea muswada huo amesema, unalenga kusaidia thamani za Ufaransa kama usawa wa kijinsia, usekurali na kung’oa mizizi ya fikra za kuchupa mipaka.

Hii ni katika hali ambayo, kupasishwa kwa muswada huo kivitendo ni kushadidisha mibinyo dhidi ya Waislamu wa Ufaransa. Kama walivyosisitiza waandamanaji katika maandamano yao mjini Paris ni kuwa, serikali ilikuwa na nyenzo za kisheria katika uwanja huo na kwamba, sheria hiyo mpya haina jingine ghairi ya kubinya uhuru wa dini nambari mbili nchini humo yaani Uislamu.

Abdallah Dhikraa, Mkuu wa Kundi la Usimamizi wa Kitaifa kwa vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu sanjari na kuashiria kwamba, mwaka uliopita wa 2020, kulitokea matukio 235 ya hujuma na madshambulio ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa ikiwa ni ongezeko la matukio 154 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake (2019), na mashambulio dhidi ya misikiti pia katika mwaka huo huo yaliongezea kwa asilimia 35 anasema: Katika kipindi hiki tahadhari kuhusiana na kueneza uongo unaohusiana na Uislamu na Waislamu na vilevile baruapepe ambazo zinachochea chuki dhidi ya Waislamu nazo ziliongezeka.

Mgawanyiko katika jamii

Sheikh Ali al-Qaradaghi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu anasema: Tunamtaka Rais Macron aheshimu na kufungamana na haki na uhuru wa mwanadamu ambavyo vimedhaminiwa hata katika tawala ambazo mifumo yake ni ya jamhuri, na aepukane na hatua ambazo zinapelekea kuigawa zaidi jamii ya Ufaransa na ambazo hazioani na maslahi ya kuishi kwa salama na amani na kuthaminiwa utukufu wa mwanadamu.

Licha ya kuwa, waandamanaji hao Jumapili ya jana waliitaka serikali kwa mara nyingine tena iachane na sheria hiyo na kutouwekea mipaka uhuru wa sasa nchini humo, lakini viongozi wa Paris si tu kwamba, wameendelea kupuuza matakwa hayo ya wananchi bali wamekuwa wakichukua hatua ambazo ni za chuki dhidi ya Uislamu.

Hii ni katika hali ambayo, katika maandamano ya siku ya Jumapili, kwa mara nyingine tena Wafaransa walionyesha kuwa, jamii ya nchi hiyo haikubaliani na utendaji huo ambao ni mchezo wa kisiasa wa viongozi wa nchi. Weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa, Rais Macron na viongozi wengine wa nchi hiyo ya bara Ulaya wanafanya hima ya kufunika mapungufu ya utendaji wao katika masuala mbalimbali na wanang’ang’ani mkondo huu wa utendji kwa minajili ya kulinda nafasi zao katika uchaguzi ujao.

3473982/

captcha