IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jamhuri ya Kiislamu ikipata ilhamu ya Ahlu-Bayt (AS) iliyarejesha nyuma majoka yenye vichwa saba ya Uistikbari

20:57 - September 03, 2022
Habari ID: 3475725
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ikipata ilhamu ya AhluL-Bayt (AS) iliyashinda na kuyarejesha nyuma majoka yenye vichwa saba ya Uistikbari na ikasonga mbele kimaendeleo.

Ayatullah Sayyiid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo alipoonana na wajumbe wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (AS) pamoja na wageni washiriki wa mkutano wa 7 jumuiya hiyo na kueleza kwamba, adhama na kupendwa Ahlul-Beiti (watu wa nyumba ya Bwana Mtume) katika Ulimwenguu wa Kiislamu ni jambo lisilo na mithili.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mbeba bendera ya Ahlul-Bayt (AS) mkabala wa mfumo wa kibeberu inaamini kuwa, katika ulimwengu wa Kiislamu hakuna mstari wa kuleta utenganisho wa kimadhehebu, kikaumu na kimbari na kwamba, huo siyo uhakika wa mambo. Ameongeza kuwa, mstari pekee wa kuleta utenganisho na ambao ni wa kweli na ndio uhakika wa mambo ni mipaka iliyopo baina ya ulimwengu wa Kiislamu na kambi ya ukafiri na Uistikbari wa kimataifa.

Ayatullah Khamenei amesema, hii leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kigezo hai na imeweza kusimama kidete na kukabiliana na aina kwa aina ya uadui na hujuma baada ya kufanikiwa kubadilika kutoka katika mche mdogo mchanga na kuwa mti mkubwa na mkongwe.

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa, kushajiisha mataifa mengine kusimama kidete mbele ya vitendo vya utumiaji mabavu ni moja ya sababu za uadui za mfumo wa kibeberu na uadui wao dhidi ya Iran na kubainisha kwamba, kusambaratishwa njama za kijinai za Marekani katika mataifa mbalimbali ambapo mfano wa wazi ni kutokomezwa kundi la kigaidi la Daesh, ni moja ya mambo yaliyowafanya maadui kuelekeza nguvu zao katika kuionyesha Iran kuwa ni tishio na kuituhumu kwamba, eti inaingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine.

4082800

captcha