IQNA

Fikra

Mwanazuoni ahimiza kuutambulisha Uislamu kwa mbinu zenye busara

17:53 - May 15, 2024
Habari ID: 3478826
IQNA - Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahl-ul-Bayt (AS) ametoa wito wa kutambulisha Uislamu kwa ulimwengu kupitia njia za kidini zenye busara na hekima.

Ayatullah Reza Ramezani alihutubia hafla ya kuzindua vitabu 15 vilivyochapishwa na viwili vya sauti vilivyotayarishwa na jumuiya hiyo katika lugha tofauti.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika katika Maonesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran (TIBF) Jumatatu alasiri.

Amesema Uislamu ni dini ya kimantiki katika nyanja za maadili na sharia na lugha ya wahyi ni ya hekima na imezingatia Fitra au maumbile asili ya mwanadamu , ambayo ni lugha ya kawaida ya wanadamu wote.

Amesema kwa kuzingatia nukta hiyo, Uislamu unapaswa kukuzwa ulimwenguni kupitia busara za kidini.

Pia alibainisha kwamba Qur'ani Tukufu si Kitabu cha watu fulani au wakati fulani, bali ni cha wanadamu wote wakati wote.

Kwingineko katika matamshi yake Ayatullah Ramezani amebainisha kuwa, Jumuiya ya Kimataifa ya Ahl-ul-Bayt (AS) imetafsiri na kuchapisha vitabu 173 katika lugha tofauti.

Amesema kwa sasa jumuiya hiyo itajikita  katika kuandika vitabu kwa lugha mbalimbali badala ya kuzingatia tu tarjuma au kufasiri.

Akizungumzia shughuli za Chuo Kikuu cha Ahl-ul-Bayt (AS) ambacho ni washirika jumuiya hiyo alisema kilianza na masomo nane na kimeongeza idadi hadi 23, yakiwemo 5 ya ngazi ya PhD.

Vitabu vilivyochapishwa vilivyozinduliwa katika hafla hiyo ya Jumatatu ni vile vya lugha za Kijerumani, Kihispania, Kiingereza, Kiitaliano, Kirusi, Kifaransa, Kiswahili, Kihausa, Kifulah na Kinyarwanda.

Maonesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran (TIBF) yalizinduliwa Jumatano iliyopita, yakikaribisha zaidi ya wachapishaji 2,500 wa Iran na 60 wa kigeni ambao wamewasilisha vitabu vyao vipya zaidi katika hafla hiyo. Yakiendeshwa chini ya kauli mbiu "Tusome na Tuunde," Maonyesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran yataendelea hadi Mei 18. Yemen imepewa hadhi ya mgeni maalum katika maonyesho hayo ya vitabu mwaka huu kwa lengo la kuimarisha utamaduni wa muqawama au mapambano ya Kiislamu.

3488342

 

Kishikizo: ahul bayt as
captcha