IQNA

Fikra za Kiislamu

Mtazamo wa Uislamu kuhusu ndoto

17:46 - September 19, 2022
Habari ID: 3475810
TEHRAN (IQNA) – Katika Qur’ani Tukufu na hadithi za Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) ndoto na athari zake zimetajwa kuwa ni muhimu.

Kuna aya nyingi ndani ya Qur'ani ambazo watu, wakiwemo mitume wa Mwenyezi Mungu, wafalme, au watu wa kawaida huota ndoto.

Hii inaonyesha umuhimu wa ndoto na jinsi zinavyohusiana na maisha ya kibinafsi na ya kijamii.

Kwa mujibu wa Mtume Muhammad (S.A.W), kuna aina tatu za ndoto: Nyingine ni habari njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nyingine hurejelea masuala ya kuudhi yanayosababishwa na Shetani, na nyingine ni kuhusu mazungumzo ya mtu binafsi. Lakini ni ndoto gani ambazo ni habari njema kutoka kwa Mungu kwa waumini?

Akirejea Aya ya 64 ya Sura Yunus, “ Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” Mtukufu Mtume (SAW) alisema habari njema ni ndoto ambayo waumini wanaona katika ulimwengu huu.

Katika Hadiyth nyingine kuhusu aya hii, Mtukufu Mtume (SAW) alisema kwamba habari njema ni Ruya as-Sadiqa (ndoto ya kweli) ambayo muumini huota au mtu mwingine ameiota kwa ajili yake.

Mtume Muhammad (SAW) pia alisema kuwa Ruya as-Sadiqa ni habari njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na sehemu ya utume.

Suala la ndoto ni muhimu sana kiasi kwamba Mtukufu Mtume (SAW.) alisema mtu ambaye haamini ukweli wa Ruya as-Sadiqa, hajamwamini Mungu na Mtume Wake kikweli.

captcha