IQNA

Fikra za Kiislamu

Barua ya kihistoria ya Imam Khomeini (RA) kwa Mikhail Gorbachev

10:57 - September 02, 2022
Habari ID: 3475719
TEHRAN (IQNA)- Mikhail Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti (Union of Soviet Socialist Republics, USSR) alifariki dunia Agosti 30 2022 katika hospitali moja mjini Moscow, Russia akiwa na umri wa miaka 91 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwa mnasaba wa kifo cha Gorbachev, tunalifanyia mapitio moja ya matukio muhimu zaidi yaliyojiri katika maisha yake ya kisiasa, ambalo ni barua ya kihistoria aliyoandikiwa na Imam Khomeini (MA). Ndani ya barua hiyo, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizungumzia masuala kadhaa ya msingi na kumpa nasaha muhimu sana Mikhail Gorbachev, akiwa kiongozi wa Muungano wa Sovieti wakati huo.

Moja ya hatua zenye taathira kubwa alizochukua Imam Khomeini katika uga wa kimataifa ilikuwa ni barua yake muhimu sana na ya kihistoria aliyomwandikia Mikhail Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Urusi ya zamani. Barua hiyo imebaki kuwa hati muhimu katika historia inayodhihirisha uono mpana na wa mbali aliokuwa nao Imam Khomeini juu ya matukio na mabadiliko ya dunia; na ilikuwa pia hatua ya kumtangazia na kumlingania Gorbachev dini na njia ya fikra ya uokovu wa mwanadamu ya Uislamu. Barua hiyo maarufu na ya kihistoria, iliyotabiri kifo cha Ukomunisti na kutilia mkazo ndani yake udharura wa Urusi kuacha kutegemea na kuiegemea Magharibi, ilitolewa Januari 1,1989; kisha ikakabidhiwa kwa ujumbe aliouteua yeye Imam Khomeini mwenyewe, ambao uliwajumuisha Ayatollah Javadi Amoli, Mohammad Javad Larijani na Bibi Marzieh Hodeidah Chi Dabagh, ambao ndio waliokwenda kuikabidhi kwa Gorbachev mjini Moscow Desemba 13, 1987.

Japokuwa barua ya kihistoria ya Imam Khomeini kwa Gorbachev ilitolewa katika hali ya kushtukiza na isiyotarajiwa, ukizingatiwa pia uchambuzi wa kina aliofanya Imam Khomeini katika barua hiyo, lakini inaonesha kuwa, chimbuko lake linarejea katika historia ya Iran na Muungano wa Sovieti. Kwa upande mmoja, barua hiyo ilikuwa hatua muhimu na ya msingi zaidi kuchukuliwa na Imam Khomeini katika suala la kuyatangaza na kuyafikisha Mapinduzi nje ya nchi; na kwa upande mwingine, lilikuwa onyo muhimu zaidi lililotolewa kuhusiana na mchakato wa mageuzi yaliyokuwa yakifanywa na Muungano wa Sovieti katika zama hizo.

Kuvunjika Umaksi

Katika barua hiyo muhimu sana, Imam Khomeini alizungumzia kusikika sauti za kuvunjikavunjika mifupa ya Umaksi, wakati Muungano wa Kisovieti ukiwa ungali moja ya madola makuu yenye nguvu duniani, Vita Baridi vikiwa bado havijaisha, Ukuta wa Berlin uliokuwa nembo ya kutenganisha Mashariki na Magharibi ukiwa bado haujaporomoka, na huku Urusi, katiba yake na watu wake wakiendelea kutawaliwa na mfumo wa Ukomunisti. Ayatullah Javadi Amoli, aliyeongoza ujumbe wa Imam Khomeini ulioelekea Moscow kumfikishia barua Gorbachev anasema: Risala yote ilikuwa ni ya kulingania Uislamu; na hii ndio maana ya msamiati 'siasa ni sawa na dini' na 'dini ni sawa na siasa'. Masuala ya kisiasa ya kiistilahi hayakuwemo hata kidogo ndani ya risala hiyo... Japokuwa ujumbe wote wa Hayati Imam (Quddisa-Sirruh) ulikuwa umejaa "siasa", lakini "siasa kiistilahi" haikutumika ndani yake.

Masikitiko ya Gorbachev

Miaka kadhaa baadaye, katika mnasaba wa kumbukumbu ya kifo cha Imam Khomeini (MA), Mikhail Gorbachev alikuja kufanyiwa mahojiano ambapo alieleza masikitiko yake kwa kupuuza maonyo na indhari alizopewa siku zile na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Gorbachev alisema: "Kwa maoni yangu, risala ya Ayatollah Khomeini ilizihutubu zama zote za historia." Akaongezea kwa kusema: “nilipopokea risala hii, nilihisi mtu aliyeandika risala hii ni mwanafikra anayeuhurumia mustakabali na hatima ya ulimwengu. Tafsiri iliyonipitikia kwa kuisoma risala hii ni kwamba, yeye ni mtu anayeuhofia ulimwengu na anapenda niyafahamu na kuyaelewa zaidi Mapinduzi ya Kiislamu."

Kuungama dhahir shahir Gorbachev kwamba utabiri wa Imam Khomeini ulikuwa sahihi ni ithibati kwamba, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa na maono, basira na utambuzi wa kina wa mambo, kwani alizitangulia kiutambuzi zama hizo kwa kutabiri kuanguka dola kuu la kambi ya Mashariki, wakati Shirikisho la Sovieti lilikuwa lingali kwenye kilele cha uwezo na nguvu.

Parstoday

 

captcha