IQNA

Serikali ya Malaysia Kuongeza Fedha kwa Ajili ya Tafsiri za Qur’ani za Taasisi ya Restu

20:25 - August 09, 2025
Habari ID: 3481060
IQNA – Waziri Mkuu wa Malaysia amesema kuwa serikali yake itatenga ufadhili wa ziada kwa Yayasan Restu ili kuwezesha tafsiri ya Qur’ani Tukufu katika lugha nyengine 30, na hivyo kupanua zaidi upeo wa ujumbe wake wa ulimwengu.

Anwar Ibrahim amesema kuwa juhudi hizi, ambazo karibuni zaidi zimeona Qur’ani ikitafsiriwa kwa lugha ya Kirusi, zinaendeleza kazi iliyopo tayari ya taasisi hiyo ya kutoa tarjuma na tafsiri katika lugha 30, na hivyo kuongeza zaidi upeo wa kufikisha ujumbe wa Qur’ani unaokubalika kwa wote duniani.

Anwar, ambaye pia ni Waziri wa Fedha, amesema hatua hii itaimarisha nafasi ya Malaysia kama miongoni mwa wachapishaji wakubwa wa Qur’ani duniani pamoja na Saudi Arabia na Misri, huku ikithibitisha uongozi wake wa kikanda katika nyanja hii.

“Kila nchi ninayoitembelea, iwe ni Peru, Brazil, Cambodia, Laos, China au Russia, sikosi kubeba Qur’ani iliyotafsiriwa ili kuikabidhi kwa serikali, kituo cha Kiislamu, au msikiti wa eneo hilo,” amesema katika hafla ya uzinduzi wa uchapishaji na tafsiri ya Qur’ani ya 30 (kwa lugha ya Kirusi), Mushaf Ummah al-Jami’, na zoezi la kupeleka kontena la Qur’ani nje ya nchi, lililofanyika Putrajaya siku ya Ijumaa.

Amesema mpango huu unaendana na mwelekeo wa serikali ya MADANI, inayosisitiza uenezaji wa da‘wah kwa hekima na kwa msingi wa elimu na uelewa, ili kupinga ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) katika ngazi ya kimataifa.

Kwa ufadhili huu wa ziada, Yayasan Restu, inayoongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wake na Mkurugenzi Mkuu wa Nasyrul Qur’an, Abdul Latiff Mirasa, inalenga kuongeza idadi ya tafsiri za Qur’ani kufikia lugha 60 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Wakati huohuo, Anwar amesema kuwa Mushaf MADANI, unaotarajiwa kuzinduliwa mwezi wa Ramadhān mwakani, umechochewa na uzoefu wake huko Jakarta, Indonesia, aliposhuhudia miswada ya Qur’ani iliyopambwa kwa mitindo ya sanaa za kienyeji kutoka maeneo mbalimbali nchini humo.

Amesema mbinu hii haiakisi tu ujumbe wa kiulimwengu wa Qur’ani, bali pia inaheshimu urithi wa tamaduni ambazo hazipingani na roho ya Kitabu Kitukufu.

“Nilipokuwa katika Msikiti wa Istiqlal mjini Jakarta wakati wa utawala wa Rais Soeharto, niliona miswada ya Qur’ani ikiwa na mapambo ya mitindo ya sanaa za kienyeji kutoka maeneo kama Minang, Palembang, Kijava, Kibatak na Kisunda. Yote haya yanaonesha ujumbe wa kiulimwengu wa Qur’ani,” amesema Anwar.

Kuhusu jitihada za  tarjuma au tafsiri, Anwar amepongeza pande zote zilizoshirikiana, hususan Naibu Waziri Mkuu Ahmad Zahid Hamidi, kwa kuendeleza mradi huo hata katika nyakati ambazo hakuwa serikalini.

“Kwa msaada endelevu wa serikali ya MADANI, tuna imani kuwa dhamira hii tukufu itafikia viwango vya juu zaidi, ikinufaisha si Waislamu pekee bali pia binaadamu wote kwa jumla,” amesema.

/3494167

Habari zinazohusiana
Kishikizo: malaysia qurani tukufu
captcha