IQNA

Vitisho vya kuwaua Waislamu Sydney baada ya mpanga wa kuadhini mwara moja kwa wiki

20:16 - August 09, 2025
Habari ID: 3481059
IQNA – Viongozi wa moja ya misikiti mikubwa zaidi nchini Australia wamesema wamepokea vitisho vya kuuwawa baada ya kutangazwa mpango wa kuweka vipaza sauti vipya kwa ajili ya adhana.

Msikiti wa Lakemba, ulioko magharibi mwa jiji la Sydney, umeimarisha ulinzi wake, ikiwemo kufunga kamera za ziada za ulinzi (CCTV), kufuatia vitisho vilivyohusishwa na pendekezo la gharama ya dola 22,000 la Chama cha Waislamu wa Kilebanoni (Lebanese Muslim Association – LMA).

Mpango huo unalenga kuongeza vipaza sauti vinne katika minara ya msikiti ili kutangaza adhana mara moja kwa wiki, siku ya Ijumaa, kwa muda usiozidi dakika 15.

Katibu wa LMA, Gamel Kheir, amesema kuwa jambo lililoanza kama ombi la kawaida la maendeleo sasa limegeuka kuwa mzozo mkali, na jumbe za matusi kumiminika.

“Kuna pingamizi ambazo, kwa hali mbaya zaidi, zinatokana moja kwa moja na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia),” amenukuliwa na gazeti la WA Today siku ya Jumamosi.

Ameongeza kuwa kauli zinazotolewa mara nyingi hurudia dhana isiyo na msingi kwamba “Waislamu wanataka kuteka eneo” au kwamba wito wa swala (Adhana) unahusishwa na “tishio la kigaidi.”

Kheir ameweka wazi kuwa msikiti huo umekumbwa na vitisho tangu mashambulio ya 9/11, lakini amesema kuwa jumbe za sasa zimefikia “kiwango cha juu zaidi.”

Aidha, amehoji kwa nini kengele za makanisa katika maeneo mengine ya Sydney hazileti upinzani kama huu, ilhali pingamizi nyingi hutoka kwa watu wasiokaa katika eneo la Canterbury-Bankstown.

Halmashauri ya Canterbury-Bankstown itajadili pendekezo hilo katika kikao cha jopo la upangaji miji wiki ijayo. Ripoti ya halmashauri imehitimisha kwamba, ingawa vipaza sauti vinaruhusiwa chini ya mpango wa matumizi ya kidini wa eneo hilo, vingesababisha “athari kubwa za kelele” na haviwezi kuendelea kwa hali vilivyo sasa.

Uchanganuzi wa sauti katika ombi hilo umeonesha kuwa adhana inaweza kufikia kiwango cha hadi decibel 92 — sawa na sauti ya pikipiki — na kusikika ndani ya umbali wa mita 100 kutoka msikiti.

Kheir amesema kuwa LMA sasa ipo kwenye mazungumzo na halmashauri hiyo kuhusu kutoa tathmini zaidi za kelele, kwa matumaini ya kurejesha pendekezo hilo mezani. Ametilia mkazo kuwa wito wa swala utatangazwa tu kwa swala ya adhuhuri siku ya Ijumaa, na sio usiku.

Kwa mujibu wa maombi ya LMA, matangazo hayo ya adhana “yatakuza mshikamano na imani ya pamoja” kwa wakazi wengi, na kuwa “sauti ya kawaida na ya faraja” inayogusa maisha ya kila siku.

3494170

captcha