IQNA

Qur’ani Tukufu Inasemaje/12

Vigezo vya Qur’ani kuhusu kutenda mema

8:16 - October 18, 2022
Habari ID: 3475950
TEHRAN (IQNA) – Vigezo vya kutenda mema kumcha Mwenyezi Mungu vimetajwa katika aya moja ya Qur’ani Tukufu na vinaangazia mtazamo wa Qur’ani kuhusu jinsi Waislamu wanavyopaswa kuwa na tabia na imani wanazopaswa kuwa nazo.

Aya ya 177 ya Sura Al-Baqarah inaeleza haki na watu wema na kuwasilisha vigezo vya kutenda mema, ikiwa ni pamoja na kumwamini Mwenyezi Mungu, Akhera, Malaika na vitabu vya Mwenyezi Mungu pamoja na Infaq (kutoa kwa wanaohitaji), kusali, kutoa Zaka , Wafa bil-Ahd (kudumisha ahadi) na kudumisha Taqwa (kumcha Mungu).

Aya hii inasema : “Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.”

Ili kuelewa sehemu ya kwanza ya aya hii, ni vyema kufahamu maoni ya Sheikh Tabarsi (mwanachuoni wa Madhehebu ya Shia wa karne ya 12). Anasema wakati Qibla (mwelekeo ambao Waislamu husali) kilipobadilika kutoka Al-Quds hadi Ka’aba Tukufu huko Makka, mabishano yalizuka kati ya Waislamu, Wayahudi na Wakristo. Wayahudi walisema ingekuwa afadhali kusali kuelekea magharibi ilhali Wakristo walisema sala inapaswa kusemwa wakiwa wametazama mashariki. Aya hii iliteremshwa ili kusisitiza kuwa masuala haya ni ya pembezoni na lililo muhimu ni uadilifu na kutenda mema.

 Kwa mujibu wa aya hii, kuelekea mashariki au magharibi si msingi wa kutenda mema, bali kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu, Akhera, Malaika na vitabu vya Mwenyezi Mungu ndivyo muhimu zaidi. Kutenda mema ni katika kusaidia jamaa, kutoa sadaka kwa mayatima, masikini na wengine wenye mahitaji na kusaidia kuwakomboa watumwa. Mahali pengine katika aya hii, kusali, kutoa Zaka, kushika ahadi na subira ya mtu katika kukabiliana na magumu pia kunatajwa kuwa ni vigezo vya uadilifu.

Katika tafsiri nyingi za Qur’ani Tukufu, kumekuwa na Hadith kutoka kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kuhusu aya hii. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema yeyote atakayeifanyia kazi aya hii, imani yake itakamilika. Alllameh Tabatabai mfasiri maarufu wa Qur’ani aliyeandika Tafisiri ya Al Mizan anaamini kwamba wakati kukifanyia kazi kile ambacho Aya hii inakisema ni kigumu, Aya hii si ya Mitume wa Allah pekee bali pia kwa Maasumin au wasiotenda dhambi (AS) na Ulil Albab. Ulil Albab ni watu wenye akili na hekima wenye utambuzi.

captcha