IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 39

Muujiza wa Kisayansi wa Qur'ani katika Sura Az-Zumar

17:02 - November 08, 2022
Habari ID: 3476054
TEHRAN (IQNA) – Kuna mifano mingi ya miujiza ya kisayansi katika Qur'ani, ukiwemo mmoja katika Surah Az-Zumar. Hii ni miujiza kwa sababu ilitajwa katika Kitabu ambacho ni Kitakatifu karne nyingi zilizopita wakati wanadamu hawakuwa na habari nayo.

Az-Zumar ni jina la Sura ya 39 ya Qur'ani. Ina aya 75 na iko katika Juzuu za 23 na 24. Ni Makki na Sura ya 59 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW).

Zumar ina maana ya makundi ya watu, ni neno linalokuja katika aya ya 71 na 73 za Sura na inahusu kundi la watu wema wanaoingia peponi na kundi la madhalimu wanaoingia motoni. Sura pia inaeleza sifa na masharti ya makundi mawili.

Maudhui ya kimsingi katika sura hii ya Qur'ani Tukufu ni Tauhidi (itikadi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na Ikhlas (usafi wa nia). Inaanza kwa kubainisha athari za Tauhidi na inamtaka Mtume Muhammad (SAW) kuitakasa Dini yake, asiwajali miungu ya makafiri na awaambie kwamba dhamira yake ni kukuza Tauhidi na Ikhlas katika dini.

Sura Az-Zumar ina sehemu kuu kadhaa. Kualikwa kwa Tauhidi na Ikhlas ndiko kunakosisitizwa sana katika sura hii. Pia kuna umuhimu maalum unaohusishwa na Ikhlas katika kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Sura hii pia inawakosoa  wale ambao humgeukia Mwenyezi Mungu wanapokuwa katika hali ya kukata tamaa na kupoteza matumaini lakini baada ya hali zao kuwa nzuri tena husahau kila kitu.

Nukta nyingine iliyosisitizwa katika Sura hii ni suala la Siku ya Kiyama, uadilifu wa Mwenyezi Mungu, khofu ya Siku ya Kiyama na kufahamishwa wanadamu matokeo ya waliyoyafanya watu katika dunia hii.

Mada moja ya kuvutia iliyotajwa katika Sura hii iko katika Aya ya 6: "Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi?"

Baadhi ya wafasiri wa Quran wanasema mapazia matatu ya giza yanarejelea tumbo, tumbo la uzazi na amnion- utando unaofunika kwa karibu kiinitete cha mwanadamu-. Wafasiri wengine wanasema inarejelea tu amnioni ambayo hufunika kiinitete na ina tabaka tatu. Hii imetajwa kama moja ya miujiza ya kisayansi ya Qur'ani Tukufu.

Habari zinazohusiana
captcha