IQNA

Tawakkul Katika Qur’ani /10

Daraja za Tawakkul

14:08 - April 13, 2025
Habari ID: 3480532
IQNA – Baadhi ya watu humkumbuka Mwenyezi Mungu pale tu wanapojiridhisha kuwa njia zote zimefungwa. Ni pale wanapoona kuwa kila njia imezibwa ndipo huamua kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo daraja au ngazi ya chini kabisa ya Tawakkul (kumtegemea kwa Mwenyezi Mungu), na ngazi za juu hupatikana kwa kuongezeka kwa imani.

Kiongozi wa Waumini, Imamu Ali (A.S), amesema: Watu wenye imani iliyo thabiti zaidi ni wale ambao wana Tawakkul zaidi kuliko wengine; kadiri mtu anavyozidi kuwa na Tawakkul, ndivyo anavyomjua Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu zaidi, na imani yake huwa timilifu zaidi.”

Tunaweza kufikiria ngazi mbalimbali za Tawakkul, ambapo hatua tatu za awali ni hizi zifuatazo:

1. Tawakkul Katika Kukabiliana na Vikwazo
Ngazi dhaifu ya Tawakkul hutokana na uelewa kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka njia na sababu ulimwenguni, na ametupa uwezo kama vile fikra na utendaji. Hata hivyo, Yeye anaweza pia kuondoa athari na ufanisi wa uwezo huu. Aina hii ya Tawakkul humaanisha kuwa tunapotumia neema alizotupatia, tunapaswa kutambua kuwa Mungu anaweza pia kutunyima neema hizo. Kwa maneno mengine, tunapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kushinda vikwazo vya maisha.

2. Tawakkul Katika Sababu Zilizo Nje ya Mamlaka ya Binadamu
Ngazi ya juu zaidi ya Tawakkul huhusisha kuelewa kwamba mafanikio ya matamanio yetu yoyote yanahitaji masharti mengi, kati ya hayo mengi yakiwa nje ya uwezo wetu. Kwa hiyo, ili kuyafikia malengo yetu, tunatumia njia zilizoko ndani ya uwezo wetu, lakini kwa yale masharti yaliyo nje ya ufahamu wetu au mamlaka yetu, tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine, ngazi hii ya Tawakkul ni ile ya kumtegemea Mungu katika kutimizwa kwa masharti yaliyo nje ya uwezo wa mwanadamu.

3. Kuutegemea Mnyororo wa Visababishi
Mtu anaweza kufikiria kuwa sababu na athari ulimwenguni ni kama viungo vya mnyororo uliofungamana, ambapo mwisho wa mnyororo huo uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kuuweka mnyororo huu katika harakati; yaani, ikiwa Mwenyezi Mungu hatavianzisha viungo vya mwanzo vya mnyororo huu, basi hakuna litakalotendeka. Hivyo basi, ni lazima mtu awe na imani kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayesababisha mnyororo huu kuanza na kuwa na athari. Katika ngazi hii, mtu hutambua kuwa hata vile vilivyo ndani ya uwezo wake ni sehemu tu ya mnyororo ambao mwanzo wake umo katika uweza wa Mwenyezi Mungu. Bila shaka, zipo ngazi za juu zaidi za Tawakkul pia.

3492652

Kishikizo: mwenyezi mungu
captcha