IQNA

Tawakkul Katika Qur’ani/8

Kumtegemea Mwenyezi Mungu: Mafunzo kutoka kwa Manabii

11:43 - April 07, 2025
Habari ID: 3480508
IQNA – Katika Surah Hud, baada ya kueleza visa vya baadhi ya manabii wakubwa wa Mwenyezi Mungu – akiwemo Nuhu, Hud, Swaleh, na Shu’ayb (amani iwashukie wote) – na namna walivyomtegemea Mwenyezi Mungu (Tawakkul) licha ya dhuluma na mateso kutoka kwa watu wao, Qur’ani Tukufu inamaliza kwa ujumbe wa ajabu, mfupi lakini wenye uzito mkubwa wa kiroho na kielimu.

Katika surah hii, Qur’ani Tukufu inazungumzia Sunnatullah – yaani, njia ya kawaida na ya kudumu ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja Wake – kwa kupitia simulizi za mataifa yaliyopita kama watu wa Nuhu, Hud, Swaleh, Luti, Shu’ayb, na Musa, wote kwao iwe amani.

Inataja hatima ya mataifa hayo, na wakati huo huo inabainisha ahadi za Mwenyezi Mungu kwa waumini pamoja na onyo kali kwa wale waliokufuru na kuzikataa ishara Zake.

Mafundisho mengine ya kiimani kama tawhidi (umoja wa Mungu), nubuwwah (utume), na  qiyāmah (Siku ya Kiyama) yanaangaziwa pia kupitia visa hivyo, vikihusiana moja kwa moja na maana ya Tawakkul.

Katika aya ya mwisho ya surah hii tukufu, tunasoma:

“Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika ardhi na mbingu, na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda.” (Surah Hud: 123)

Katika aya mbili zilizotangulia, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume Muhammad (SAW) kutekeleza kile alichopewa kama jukumu la risala na akaambiwa avute subira kwa ajili ya ahadi ya Mola Wake. Aya hii ya mwisho inasisitiza mambo matatu makuu: Kwanza ni ujuzi wa Mwenyezi Mungu wa mambo ya ghaibu: Kwamba yote yaliyofichika katika mbingu na ardhi yapo katika ujuzi Wake kamili. Hivyo, haijalishi makafiri wanapanga nini, mipango yao haizidi mipaka ya Qudra ya Mwenyezi Mungu.

Pili ni kuwa, Mambo yote humrejea Yeye: Wanaopinga risala ya haki hudhani kuwa kwa kutumia njia zao wataweza kubadili hatima. Lakini mambo yote – ya mbingu na ardhi, ya dhahiri na ya siri – yapo chini ya Qudra ya Mwenyezi Mungu. Hatima yao inapangwa na Yeye kwa hekima Yake isiyo na mipaka.

Na nukta ya tatu ni hii kuwa, “Mwabudu Yeye na umtegemee Yeye” – Amri mbili zenye jumla ya risala nzima: Allamah Sayyid Muhammad Hussein Tabataba’i – Allah amrehemu – anasema kuwa aya hii ni katika maneno yenye uzito mkubwa katika Qur’ani, kwani imebeba ujumbe mzito wa ulinganizi wa Mtume katika maneno mawili tu: ‘fa‘budhu wa tawakkal ‘alayh’.

Hii ni kusema: mja anapaswa kujisalimisha kwa ibada kwa Mwenyezi Mungu katika kila hali ya maisha, na pia kumtegemea Yeye kwa yakini kamili, bila kuruhusu wasiwasi, hofu au tamaa ya wanadamu kudhoofisha moyo wake.

Kwa hivyo, Tawakkul ya kweli hutokana na imani ya dhati kwamba Mwenyezi Mungu anajua kila kitu (hata yale yaliyo siri kabisa), ana mamlaka juu ya kila jambo, na kwamba ibada na utiifu wa kweli kwake ni daraja ya juu ya imani. Hapo ndipo mja huacha mambo yake yote mikononi mwa Allah, huku akijitahidi kutenda kwa ikhlasi na subira.

3492598

 

Kishikizo: mwenyezi mungu
captcha