IQNA

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon

Kuna dalili ambazo hivi sasa zinaashiria kusambaratika utawala wa Israel

17:40 - March 08, 2023
Habari ID: 3476679
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema matukio na maendeleo yanayoshuhudiwa hivi sasa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni ishara tosha kuwa suala la kuporomoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni hakika ambayo itafanyika katika mustakabali wa karibu.

Sayyid Hassan Nasrallah aliyasema hayo Jumatatu katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuwaenzi Mashahidi wa Hizbullah yaliyofanyika mjini Beirut na kusisitiza kuwa, maamuzi yote yaliyochukuliwa na mamlaka za Kizayuni yanaashiria kuwa Wazayuni wapo katika mkondo aa kuporomoka na kusambaratika.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameeleza bayana kuwa, mgawanyiko ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel, ni ishara ya kuongezeka kasi ya kusambaratika utawala huo pandikizi. 

Sayyid Nasrallah amesisitiza kuwa, mapambano na muqawama ndio njia pekee ya kuikomboa Palestina na Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Amefafanua kwa kusema, "Maamuzi yanayochukuliwa na Wazayuni hayatakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuzidisha ari, imani na subira ya Wapalestina ya kuendeleza operesheni zao za kulipiza kisasi."

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Sayyid Nasrallah amelaani hatua ya serikali yenye misimamo ya kufurutu ada ya Benjamin Netanyahu ya kupasisha muswada ambao ukiidhinishwa na kuwa sheria, mamlaka za Kizayuni zitakuwa na kibali cha kuwaua wafungwa wa Kipalestina.

Amesema: Adui katili Mzayuni anadhani kuwa atawanyamazisha na kuwafumba midomo Wapalestina kwa kutishia wanajihadi na makundi ya muqawama au kuwahukumu kifo.

Sanjari na kutangaza uungaji mkono kwa wafungwa wa Kipalestina, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema umma wote wa Kiislamu una wajibu wa kuliunga mkono taifa la Palestina mkabala wa utawala wa Kizayuni.

4126478

captcha