IQNA

Muqawama

Kiongozi wa Hizbullah: Israel ni saratani ambayo ni lazima itumuliwe katika eneo

10:54 - June 01, 2024
Habari ID: 3478910
IQNA-Kiongozi wa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ametaka juhudi za kimataifa za kuutokomeza utawala wa Kizayuni, akisema ni utawala huo ni 'uvimbe wa saratani" ambao lazima uondolewe.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni Ijumaa,  Sayyed Hassan Nasrallah alisema kuwa mapambano yanayoendelea kwa ajili ya Gaza ni vita vya uwepo, na kushindwa kwa utawala wa Israel katika vita hivyo kutakuwa na taathira chanya kieneo.

Ameongeza kuwa pamoja na kwamba baadhi ya serikali zimenyamaza kimya kutokana na ukatili wa utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina  huko Gaza, lakini vita hivyo vimeamsha maoni ya umma wa kimataifa na kuutenga utawala huo ghasibu.

Vile vile amezungumzia mapigano ya hapa na pale  yanayoendelea kati ya Hizbullah na utawala ghasibu wa Israel na kusema  vita vya Gaza vinahusiana na mustakabali wa Lebanon na eneo zima katika ngazi za kistratijia, usalama na kitaifa.

Kwingineko katika matamshi yake, kiongozi wa Hizbullah amepongeza operesheni za Majeshi ya Yemen dhidi ya Israel, huku akionyesha mshikamano na wananchi na jeshi la Yemen katika kukabiliana na hujuma za Marekani na Uingereza dhidi yao.

Amepongeza uthabiti wa Wayemeni katika juhudi zao za kuunga mkono Wapalestina wa Gaza na ahadi yao kwamba hakuna shinikizo lolote linaloweza kusimamisha operesheni zao dhidi ya Israel.

Sayyed Nasrallah pia ameashiria maandamano ya wanafunzi wanaounga mkono Palestina nchini Marekani, akisema yamepanua wigo wa muqawama na harakati za mapambano dhidi ya ubeberu katika nchi za Magharibi.

3488577

Habari zinazohusiana
captcha