"Tuna uhakika kabisa wa kupata ushindi," imesema taarifa iliyotolewa leo Jumatano ya harakati hiyo.
Taarifa hii ya Hizbullah imetolewa baada ya milipuko iliyotokea kwa wakati mmoja kote Lebanon siku ya jana Jumanne.
Kulingana na taarifa, Shirika la Ujasusi la Israel Mossad lilitega viripuzi kwenye vifaa vya 'pager' vilivyoripuka jana Jumanne nchini Lebanon, na kuua watu 13, akiwemo mtoto, na kujeruhi karibu wengine 3,000 , wakiwemo 200 ambao hali zao ni mahututi.
Pager ni kifaa cha mawasiliano ya simu kisichotumia waya ambacho hupokea na kuonesha jumbe za alphanumeric au sauti.
Hapo awali, Hizbullah ilisema kwamba, baada ya kuchunguza ukweli wote na taarifa zilizopo kuhusu mashambulizi hayo, inautambua utawala wa Israel kuwa "unawajibika kikamilifu kwa jinai hiyo."
Hizbullah imesema "Muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon utaendeleza operesheni zake zilizobarikiwa za kuunga mkono Gaza, watu wake, na mapambano ya ukombozi wa Palestina."
"Operesheni hizo pia zitafanyika kutetea Lebanon, watu wake, na uhuru wake," imeongeza taarifa hiyo.
Hizbullah imekuwa ikifanya mashambulizi karibu ya kila siku dhidi ya Israel ikiwa ni kuunga mkono na kuwatetea watu wa Ukanda wa Gaza na mashambulizi makali ya Israel ambayo yamekuwa yakilenga ardhi ya Lebanon tangu kuanzishwa kwa vita mauaji ya kimbari katika ardhi ya Palestina.
3489943