IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 105

Sura Al-Fil: Nguvu ya Mwenyezi Mungu inavyoonyeshwa na Ndege

18:10 - August 12, 2023
Habari ID: 3477426
TEHRAN (QNA) – Miezi michache kabla ya kuzaliwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW), mfalme wa wakati huo wa Yemen alitaka kuiangamiza Ka’aba Tukufu lakini Mwenyezi Mungu alidhihirisha uwezo wake kwa njia ya muujiza na akazuia hilo lisitokee. Hayo ni kwa mujibu wa Sura Al- Fil katika Qur'ani Tukufu.

Al-Fil ni sura ya 105 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 5 na iko katika Juzuu ya 30. Ni Makki na ni Sura ya 19 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Inahusu ‘watu wa tembo’ au ‘wamiliki wa tembo’ – kundi la watu ambao, wakiwa wamepanda tembo walitaka kuibomoa Ka’aba takatifu – na kwa hiyo jina la Sura limetokana na kisa hicho.

Ni tukio la kihistoria ambalo Mwenyezi Mungu aliiokoa Ka’aba kutoka kwa jeshi la makafiri waliokuwa wametoka Yemen wakiwa wamepanda tembo au ndovu. Kuashiria hadithi hii ni onyo kwa maadui  wa Uislamu ili watambue kuwa hawana uwezo mbele ya uwezo mkubwa wa Mwenyezi Mungu.

Mtu aliyetaka kuibomoa Ka’aba alikuwa ni Abraha, mfalme wa Yemen. Alipojua juu ya hadhi muhimu ya Makka ambayo ilitembelewa na Mahujaji kutoka kila mahali, alijenga kanisa kubwa ili watu walitembelee badala ya Ka'aba lakini sio watu wengi waliokwenda kutembelea kanisa hilo. Ndiyo maana alikusanya jeshi la wapiganaji waliokuwa wamepanda ndovu kuelekea Makka.

Watu wa Makkah, kwa kuhofia maisha yao, wakaondoka mjini.

Asubuhi iliyofuata, wakati Abraha alipoanza kushambulia Makka, idadi kubwa ya ndege walikuja, ambao kila mmoja alileta mawe matatu madogo. Walidondosha mawe juu ya askari wa Abraha. Kila aliyepigwa na mawe haya aliuawa, akiwemo Abraha mwenyewe.

Inasemekana kwamba tukio hilo lilitokea mwaka wa 570 Miladia, unaojulikana kwa jina la Aam al-Fil (mwaka wa tembo).

Ni mwaka ambao Mtume Muhammad (SAW) alizaliwa.

Zifuatazo ni aya za Sura Al Fil

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu

1.Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo?

2. Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika? 

3. Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi, 

4. Wakiwatupia mawe ya udongo wa Motoni, 

5. Akawafanya kama majani yaliyo liwa! 

Kishikizo: SURA ZA QURANI
captcha