IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /17

Miujiza Tisa ya Nabii Musa katika Surah Al-Isra

14:36 - July 10, 2022
Habari ID: 3475483
TEHRAN (IQNA) – Hadithi za Nabii Musa (AS) zimesimuliwa katika sura tofauti za Qur’an, ikiwa ni pamoja na Sura Al-Isra, ambamo miujiza 9 ya Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu imetajwa.

Surah Isra, pia inajulikana kama Bani Israil, ni sura ya 17 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 111 na iko katika Juzuu ya 15. Ni Sura ya 50 iliyoteremshwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Aya mbalimbali za sura hii zinazungumzia mada kama vile Tauhidi, Siku ya Kiyama, kukataa au kupinga Shirki (shirki), Mi'raj (kupaa mbinguni) ya Mtukufu Mtume Muhammad SAW, ushahidi wa utume, miujiza ya Qur'anI, na jinsi dhambi atendazo mwanadamu zinaweza  kuathiri imani yake,

Jina la Sura hii, Al-Isra, linarejelea safari ya usiku ya Mtukufu Mtume (SAW) kutoka Msikiti Mkuu wa Makka hadi Msikiti wa Al-Aqsa huko Al-Quds (Jerusalem). Baadhi ya aya za mwanzo na mwisho wa Sura zinasimulia kisa cha Bani Israil.

Mwanzoni mwa Sura, Qur'ani Tukufu inaashiria namna Bani Israel walivyoeneza ufisadi duniani na Bani Israili. Mungu anawaonya juu ya matokeo na adhabu inayowangoja kutokana na hili. Aya zilizoko mwishoni mwa Sura hiyo zinabainisha miujiza 9 ya Nabii Musa (AS) pamoja na mjadala wake na Firauni, kuzama kwa Firauni na waliomfuata, na makazi ya Bani Israil huko Misri.

Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, Nabii Musa (AS) alikuwa na miujiza 9: Kugeuza fimbo yake kuwa nyoka, na kuingiza mkono wake ndani ya nguo zake, na kuangaza mwanga mkubwa wakati alipoifunua, kukabiliana na dhoruba, nzige kushambulia mashamba, Qummul (wadudu waharibifu wa mimea), vyura, maji ya Mto Nile kubadilika kuwa damu, ukame, na kuzama kwa Firauni na jeshi lake.

Tafsiri ya Nemouneh ya Qur'ani Tukufu imetaja masuala ya kiitikadi, kimaadili na kijamii yaliyojadiliwa katika Sura hii kuwa ni muhimu sana kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa watu katika maeneo mbalimbali.

Sura pia inazungumzia mada ya kifalsafa kuhusu mwenendo wa mwanadamu na suala la hiari. Sura hii inasema mwanadamu anaweza kutenda mema au mabaya na ataona matokeo ya matendo yake. Kwa hiyo mwanadamu ana hiari ya kuchagua njia yake.

“(Tuliwaambia), Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa.” ( Al Isra Aya 7).

Miongoni mwa masuala mengine yaliyotajwa katika Sura hii ni sababu ya kuwepo mchana na usiku, kumshukuru baba na mama, ukweli kwamba yale aliyoyafanya mwanadamu hapa duniani yatapitiwa upya Akhera, haja ya kuwasaidia wengine na kuepuka ubadhirifu. ubahili, kiburi na ukaidi.

Habari zinazohusiana
captcha