IQNA

Habari njema ya Qur'an kuhusu ulimwengu unaotawaliwa na watu wema

15:40 - February 22, 2024
Habari ID: 3478397
IQNA - Kama vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyotangulia, Qur'ani Tukufu inatoa habari na bishara njema ya kuundwa kwa serikali ya ulimwengu yenye umoja duniani ambayo itaongozwa na watu wema na waliokuwa wamedhulumiwa na kukandamizwa.

Makumi ya aya za Qur'ani Tukufu zimeangazia kadhia ya ujio wa mwokozi. Mtazamo wa nyingi ya aya hizi ni juu ya kuwapa habari njema watu wema na wanaodhulumiwa juu ya kupata tena haki zao na kuundwa serikali ya ulimwengu kwa misingi ya ukweli na uadilifu ambapo Uislamu utaweza kuwa na hadhi ya juu zaidi ya dini au itikadi zingine zote.

Qur’an inasema bishara hii njema imetajwa katika vitabu vingine vya Mwenyezi Mungu;

 “ Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema." ( Aya ya 105 ya Surah Al-Anbiya).

Vile vile Qur'ani Tukufu inahusisha bishara hii na mapenzi ya Mwenyezi Mungu: “Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika nchi hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi." (Aya ya 5 ya Surah Al-Qasas)

Katika aya nyingine, wametajwa watu wema na Waumini wanaorithi ardhi kuwa ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa Waumini: “Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu. (Aya ya 55 ya Surat An-Nur)

Mbali na aya zinazozungumzia ujio wa mwokozi, kuna karibu Hadith 100 zilizosimuliwa na masahaba 20 wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) ambazo zimetajwa katika vyanzo vingi vya Hadithi vya Sunni.

Muslim na Bukhari wote wamesimulia Hadith ambayo kwayo Mtukufu Mtume Muhammad  (SAW) alisema: “Mtakuwaje atakaposhuka mwana wa Maryamu (yaani Isa) miongoni mwenu na imamu wenu akiwa miongoni mwenu.”

Pia,  Muslim ibn al-Hajjaj al-Naysaburi amemnukuu Jabir akisema kwamba alimsikia Mtukufu Mtume (SAW) akisema: “Kamwe hapatakosekana kuwa kundi ndani ya Ummah wangu ambalo litakuwa linapigania Haki, lenye ushindi hadi Siku ya Qiyaamah. Kisha, ‘Isa bin Maryam (AS), atashuka, na Amir wao atasema, ‘Njoo utuongoze katika swala.’ Lakini, yeye (‘Isa) atajibu, ‘Hapana. Hakika baadhi yenu ni maamiri wa wengine. Huu ni utukufu wa Mwenyezi Mungu kwa Ummah huu.’”

Sheikh Mansour Ali Nasif ameandika katika kitabu Al-Taaj: “Miongoni mwa wanachuoni wote wa leo na waliopita inajulikana kwamba hatimaye atatokea mtu kutoka miongoni mwa Ahl-ul-Bayt wa Mtukufu Mtume (SAW) ambaye atatawala ardhi zote za Waislamu na Waislamu watamfuata. Atasimamisha uadilifu baina yao na atainua dini.”

Kwa hivyo inapaswa kusemwa kwamba madhehebu zote za Kiislamu zinanaamini kwamba mtu kutoka katika kizazi cha Mtukufu Mtume (SAW) ataongoza mwamko wa kimataifa katika zama za mwisho ili kusimamisha uadilifu duniani kote.

Aya za Qur'an na Hadithi zinaonyesha kwamba kwa mujibu wa hekima na rehema za Mwenyezi Mungu, viongozi watakatifu katika historia daima wamekuwa wakiwapa watu habari njema na maonyo na daima kumekuwa na kiongozi ambaye ni mja mwema wa Mwenyezi Mungu katika ardhi. Kwa hivyo mwokozi aliye na hadhi ya kuwaongoza watu siku moja atadhihiri tena.

3487261

Kishikizo: mwokozi imam mahdi
captcha