IQNA

Vita vya siri vinavyolenga kuzuia Kuenea kwa itikadi ya Imam Mahdi katika nchi za Magharibi

17:14 - February 15, 2025
Habari ID: 3480222
IQNA – Binadamu wote wanatarajia kuonekana kwa Mwokozi mwishoni mwa nyakati, lakini kuna watu ambao maslahi yao yanapingana na tukio hili, hivyo wanajitahidi kwa bidii na kwa  siri kudhoofisha na kuondoa imani ya kuonekana kwa Mwokozi.

Haya ni kwa mujibu wa Mujtaba al-Sada, mtafiti na mwandishi wa Kishia kutoka Saudi Arabia, akizungumza katika makala kuhusu vita vya siri dhidi ya Imam Mahdi (Mungu aiharakishe kudhihiri kwake).

Hapa chini ni baadhi ya nukuu kutoka kwa makala yake:

Binadamu wote wanatarajia kuonekana kwa Mwokozi mwishoni mwa nyakati na kuanzishwa kwa haki duniani kote.

Dhana ya kungoja inahusishwa na kina cha mawazo ya binadamu na misingi na maadili ya juu. Hata hivyo, kwa kweli, asili ya matarajio haya inatofautiana kati ya watu na vikundi, kulingana na maadili, malengo, na maslahi wanayoshikilia.

Tunaona watu ambao wana hamu isiyoelezeka ya kumwona Imamu huyo anayeng'ara (Imam Zaman au Imam Mahdi) na kutamani kuishi katika serikali ya haki ya kimungu, hivyo wanajitahidi kuunda mazingira kwa ajili ya kuonekana kwa mwokozi wa mwisho wa nyakati. Kwa upande mwingine, kuna wale ambao maslahi yao yanapingana na kuonekana au kudhihiri mtukufu huyo, hivyo wanaunda vikwazo kuhusu uelewa wa kadhia hii. Wanajitahidi kwa bidii na kwa siri kudhoofisha wazo la kuonekana kwa mwokozi na kuondoa imani hii.

Vita hivi vya siri vinaweza kuwa vya kiitikadi, kiutamaduni, au kisiasa, na wakati mwingine huchukua sura ya mgogoro wa kijeshi usio wa moja kwa moja. Katika aina hii ya vita, kukabiliana na mgogoro na upande unaopingana hakuanzi rasmi, lakini hufanywa kwa siri kwa kutumia mbinu kama udanganyifu, upotoshaji, ushawishi, na zaidi, bila kuweka wazi malengo.

Matukio ya Septemba 11, 2001, na Vita vya Iraq mnamo 2003 yalibaini mabadiliko muhimu katika vita vya siri dhidi ya Umahdi. Mashambulizi dhidi ya Imam Mahdi (AS) yaliongezeka ikilinganishwa na miongo iliyopita, na maadui walifanya vitendo vyao wazi zaidi. Mashambulizi haya yalifikia kilele chake katika kulipuliwa kwa kuba ya Haram ya Al-Askari nchini Iraq katika mji wa Samarra mnamo 2006.

Vitendo hivi vya siri vya hivi karibuni dhidi ya Umahdi, vilivyofanywa kwa njia isiyo ya moja kwa moja, vimepangwa na kusimamiwa na nguvu zisizoonekana zinazoandaa na kupanga njama.

Mtu yeyote ambaye maslahi yake yanapingana na misingi ya haki ya kimungu na ambaye anaogopa Mwokozi wa kimungu hatamani kuonekana kwake. Vivyo hivyo, mtu yeyote mwenye misingi na malengo yanayopingana na ya Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aiharakishe faraja yake) ana chuki na uadui kwake.

Pia, mtu yeyote anayeamini kuwa kuanguka kwa utawala wake kutakuwa mikononi mwa Imam Mahdi (AS) atampinga hata kabla ya kuonekana kwake.

Sababu halisi na motisha za kuendesha vita dhidi ya Imam Mahdi (AS) kimsingi ni vita dhidi ya imani za Kiislamu.

Upinzani dhidi ya Umahdi ni mgogoro wa zamani ulioanza Magharibi kwa misingi ya kiitikadi. Hata hivyo, kwa miaka na uzoefu unaozidi kuongezeka, wapinzani sasa wamekuwa na uhakika kwamba Umahdi ni kikwazo kikubwa kwa maslahi na malengo yao, Magharibi na Mashariki ya Kati.

Bila shaka, kuna sababu nyingi za hofu na wasiwasi wa imani ya Umahdi na shakhsia ya Imam Mahdi (AS). Hata hivyo, motisha hatari zaidi ya hizi, ambayo inazidi kuchukua nafasi muhimu katika kuundwa kwa vita vya siri, inaweza kutambulika kama hofu ya Umahdi katika siku zijazo, hofu ya nguvu ya imani ya Umahdi, na hofu ya kuenea kwa misingi na maadili ya Umahdi katika nchi za Magharibi.

3491864

Kishikizo: imam mahdi
captcha