IQNA

Fasihi na Qur'ani

Hafez anawabainisha wanafiki kama 'Tishio Kubwa Zaidi' kwa Uislamu

23:49 - October 13, 2024
Habari ID: 3479590
IQNA – Akitafakari kazi za Hafez Shirazi, malenga mtajika wa Iran wa karne ya 14, profesa mashuhuri wa Iran anaangazia jinsi Hafez anavyolaani vikali uongo na unafiki, akibainisha unafiki kuwa tishio kubwa zaidi kwa Uislamu.

Fathollah Mojtabaei, profesa mstaafu wa Dini na Falsafa za Mashariki, alizungumza na IQNA hivi karibuni katika maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Hafez ambayo iliadhimishwa tarehe 11 Oktoba.
"Tunapozungumzia unafiki, tunaona namna tabia hii mbovu ilivyo adui mkubwa wa Hafez," alisema Profesa Fathulla Mojtabai katika mazungumzo hayo  na IQNA ambayo pia yalimjumuisha Ahmad Masjed-Jamei, Naibu Mkuu wa Kituo cha Insaiklopidia Adhimu ya Kiislamu ambaye aliwahi kuwa waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Iran.
"Hafez anabainisha mara kwa mara kwamba wale wanaoswali au kusoma Qur’ani kwa kujifanya au kujionyesha mbele ya watu ni wanafiki na hao ndio tishio kubwa kwa Uislamu," Mojtabaei aliongeza.
Malenga Khaja Shamsuddin Muhammad Hafez (Hafidh) Shirazi, ambaye ni maarufu kama Hafez alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia huko Shiraz moja kati ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu wa tafsiri ya Qur'ani, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafidh kutokana na kuhifadhi kwake Qur'ani Tukufu kwa visomo tofauti.
Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan.
Ushairi wa Hafez unachukuliwa kuwa kilele cha fasihi ya Kiajemi na bado unasomwa na kuheshimiwa sana nchini Iran na kwingineko duniani.
Mkusanyiko wake wa mashairi unajulikana kama Diwani ya  Hafez na unaendelea kuwatia moyo wasomaji na ufahamu wake wa kina.
“Hafez alikuwa mcha Mungu katika maana ya kidini; ushawishi wa Qur'ani umeenea sana katika ushairi wake," aliongeza profesa huyo mwenye umri wa miaka 96, akibainisha kuwa mshairi huyo alikuwa mfuasi wa Malamatiyya na aliitazama Qur’ani kwa mtazamo wa fikra hii.
"Katika mfumo wa imani ya Malamatiyya, unafiki na uwongo huchukuliwa kuwa dhambi kubwa na mfuasi wa kweli wa Malamatiyya kamwe hawezi kusema uwongo," aliongeza.
Katika utamaduni wa kale wa Iran, uwongo ulionekana kama kielelezo cha uovu, alisema, na kuongeza kwamba Hafez aliamini kwamba uwongo sio tu juu ya maneno lakini pia juu ya vitendo, ambapo unafiki kimsingi ni tabia ya kutenda mambo kwa msingi uwongo.
Katika Qur’ani, uwongo unakatazwa sana, alisisitiza profesa; "Na kisha, sisi kama Waislamu, tunawezaje kusema uwongo!" aliongeza
Mojtbaei aidha amesema: "Kwa ufahamu wangu, hakuna mshairi mwingine, iwe katika fasihi ya Kiajemi au zaidi, ambaye amepanua maana ya mapenzi na unafiki kwa kiwango alichofanya Hafez.”
"Unafiki umetusumbua, na Hafez alitambua suala hili kwa ufahamu wa ajabu, akitoa baadhi ya ukosoaji wenye nguvu zaidi wa unafiki, haswa kati ya tabaka la kidini," profesa huyo alibainisha.
"Katika karne ya 21, bado tunateseka na unafiki; ni ubaya wa milele," alisema na kuongeza, "Katika kazi za Hafez, tunamwona mara kwa mara akiwahutubia watu kama masheikh, mfalme, na wengine, akiwahimiza wasiwe wanafiki, wasiue, na wasidanganye. Kauli hizi zinaonyesha wasomi katika historia ya kitamaduni ya Iran walipinga vikali uongo na unafiki.
Ushairi wa Hafez unawavutia wote
"Tofauti na kazi za washairi wengine wengi, ushairi wa Hafez hauna mwelekeo mmoja," Mojtbaei ameandika katika utangulizi wa kitabu kuhusu Hafez.
 "Haizungumzii mada moja tu. Ushairi wake unajumuisha wigo mpana unaowavutia wasomi na watu wa kawaida, wa kidini na wasio wa kidini, hata wale walio na imani potofu," anaongeza.
“Beti za Hafez zinaangazia watu wote na viwango vyote vya fikra, maarifa na hisia, zikitoa kitu kwa kila mtu kulingana na uzoefu na hisia zake,” anabainisha na kuongeza, “Ushairi wa Hafez ni kama kioo ambacho kila mtu anajiona ndani yake.”

 

 

3490250

Kishikizo: malenga qurani shiraz
captcha