Kufa shahidi maana yake ni kupoteza maisha katika njia ya Mwenyezi Mungu, na yeyote anayeuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu anaitwa Shahidi.
Kuuawa au kufa kishahidi ni mojawapo ya fadhila zilizotukuka zaidi za mwanadamu na aina bora zaidi ya kifo.
Katika aya za Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtukufu Mtume (SAW), hadhi ya mashahidi imetukuka kiasi kwamba kila Muislamu anatamani kuipata.
Hadhi kama hiyo huleta haki ya shifaa, maisha yaliyotukuka, na msamaha wa dhambi, miongoni mwa mambo mengine.
Katika Kiarabu, neno Shahid (shahidi) maana yake ni yule aliyekuwepo na anashuhudia. Shahidi anaitwa Shahid kwa Kiarabu kwa sababu, ingawa tunadhania kuwa amekufa, yeye yupo, anatushuhudia, na atashuhudia matendo yetu Siku ya Kiyama.
Kwa mujibu wa Mafaqihi, mwili wa shahidi hauhitaji Ghusl na Kafan (kuoshwa na kuvikwa sanda), na mtu akiugusa mwili, hana haja ya kufanya Ghusl ya Mayyit. Hili linawahusu tu mashahidi wanaouawa kwenye uwanja wa vita pamoja wakipambana na makafiri.
Quran inataja kifo cha kishahidi kama "kuuawa kwenye njia ya Mwenyezi Mungu". Kwa mfano, Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 154 ya Surah Al-Baqarah: “Wala msiseme kuwa wale walio uwawa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti; bali hao ni wahai, lakini nyinyi hamtambui."
Wafasiri wa Qur'ani wanasema kwamba kwa kuzingatia aya hii, mashahidi wako hai katika dunia hii, wanashuhudia matendo yetu na wako pamoja nasi ingawa hatuoni uwepo wao.
Hili linasisitizwa katika Aya nyingine pia: “Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi.” (Aya ya 169 ya Surah Al Imran)
Maana ya mashahidi kuwa hai sio tu kuhusu maisha ya baada ya kifo huko Barzakh. Kwa kuzingatia aya za Qur'ani, watu wote wana maisha baada ya kifo na kila mtu ataendelea kuishi baada ya kuondoka hapa duniani. Hata hivyo, ukweli kwamba wafia imani wako hai humaanisha kwamba wako hai katika ulimwengu huu na wana ushawishi. Wanaweza kusaidia watu dhaifu, kugusa mioyo yetu, na kutuongoza kwenye njia iliyo sawa. Wako hai kwa maana ya kweli ya neno hili, na ushawishi wao juu ya ulimwengu wetu uko wazi kabisa.
3490665