IQNA

Watoto Waislamu wa Brazil Waanza Kozi ya Kuhifadhi Qur’ani huko Sao Paulo

19:14 - December 27, 2025
Habari ID: 3481721
IQNA – Kituo cha Kiislamu cha Vila Cajon kilichoko Sao Paulo, mji mkuu wa kiuchumi wa Brazil, kimeandaa kozi ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu kwa watoto.

Kozi hii imeanzishwa kwa lengo la kuimarisha utambulisho wa Kiislamu na kusimika thamani za kielimu miongoni mwa vizazi vipya vya Waislamu nchini Brazil, kwa mujibu wa tovuti ya Muslimsaroundtheworld.

Kozi hii imepokelewa kwa shangwe na watoto Waislamu. Shughuli zake, zilizoanza takriban mwezi mmoja uliopita, zitaendelea hadi mwisho wa mwezi Januari. Mwishoni mwa kozi kutafanyika sherehe kubwa ambapo zawadi za thamani zitakabidhiwa kwa washiriki waliobobea na wengineo.

Darasa hizi hufanyika kila Jumanne na Ijumaa kuanzia saa 12 jioni hadi saa 3 usiku kwa saa za eneo, na Jumatano na Alhamisi kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana, katika mazingira ya kielimu na kijamii yenye upekee.

Kozi hii inajumuisha mafundisho ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu, kanuni za Tajwid, na ufafanuzi wa Hadith Arobaini zilizoteuliwa za Mtume Mtukufu Muhammad (SAW). Aidha, masomo ya teolojia, fiqhi, na maadili pamoja na programu za kielimu kwa watoto na vijana pia yanatolewa.

Hadi sasa, wanazuoni kadhaa, wahubiri na wazee wa jamii ya Kiislamu nchini Brazil wamekuwa wakitoa mihadhara katika kozi hii chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Abdul Hamid Mutawalli, mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Kimataifa cha Toleransi na Amani nchini Brazil na Amerika ya Kusini.

Miongoni mwao ni Sheikh Ali Al-Khatib, mwakilishi wa Mamlaka ya Fatwa ya Lebanon nchini Brazil na Amerika ya Kusini, Sheikh Mukhtar, mjumbe wa Al-Azhar katika misikiti ya Brazil, na Sheikh Muhammad Buz Al-Asal, mwalimu wa kuhifadhi Qur’an na kanuni za Tajwid.

Kwa mujibu wa Abdul Hamid Mutawalli, shughuli hizi za kielimu na mafunzo ndizo nguzo kuu za kusimika thamani sahihi za Kiislamu na kuimarisha utambulisho wa kidini kwa vizazi vipya na watoto wa jamii ya Kiislamu, hususan katika mazingira yenye tamaduni mchanganyiko.

Kozi hii imekaribishwa sana na washiriki kutokana na mpangilio wake makini, maudhui ya kielimu yenye nguvu, na roho ya udugu iliyowaunganisha watoto wa jamii ya Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Sao Paulo.

3495856

Habari zinazohusiana
Kishikizo: brazil waislamu
captcha