IQNA

Zabuni za huduma za Iftar zatangazwa kwa Ramadhani katika Misikiti ya Makkah na Madinah

13:09 - December 29, 2025
Habari ID: 3481733
IQNA – Kampuni zinazobobea katika huduma za chakula kwa wingi zinakaribishwa kuomba nafasi ya heshima ya kutoa futari katika Msikiti Mtukufu wa Makkah (Masjid al Haram) na Msikiti wa Mtume (SAW), Al Masjid An Nabawi mjini Madinah wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani 2026.

Mamlaka Kuu ya Kusimamia Masuala ya Msikiti Mtukufu na Msikiti wa Mtume imetangaza kufunguliwa kwa maombi ya kampuni na viwanda vinavyotaka kushiriki katika huduma za futari katika misikiti hiyo miwili mitukufu. Hatua hii ni sehemu ya juhudi za mamlaka kuandaa huduma za futari na kuboresha ubora wa chakula kinachotolewa kwa waumini wanaoswali katika Haramain.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, waombaji wanatakiwa kutimiza masharti kadhaa, ikiwemo kuwa na usajili halali wa kibiashara, leseni ya manispaa au leseni ya Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Saudia (SFDA) kwa kituo kinachofanya kazi Makkah au Madinah.

Aidha, lazima wawe na kituo cha kazi kilicho wazi katika mojawapo ya miji hiyo miwili, chenye uthibitisho wa umiliki au mkataba wa upangaji uliothibitishwa. Taasisi husika pia inapaswa kuwa na rekodi safi ya afya ya umma, kufuata viwango vya chakula vilivyoidhinishwa na SFDA, na uwezo wa kutoa angalau futari 10,000 kwa siku.

Mamlaka imeeleza kuwa uwasilishaji wa nyaraka utaendelea hadi Rajab 10, 1447 Hijria, sawa na Desemba 30. Kampuni na viwanda vinavyovutiwa vinashauriwa kupitia kwa makini masharti yote na kuhakikisha mahitaji yote yametimizwa ndani ya muda uliowekwa.

3495885

captcha