Sheikh Saeed, aliyepata umaarufu mkubwa kwa usomaji wake wa kipekee wa Surah Yusuf, na kuwasisimua mamilioni ya wapendao Qur’an ndani ya Misri na ulimwengu wa Kiislamu, ameaga dunia jana Jumamosi.
Mwili wake utazikwa katika kijiji chake cha asili cha Meet Selsil, mkoa wa Dakahlia.
Sheikh huyu aliye kuwa mnyenyekevu alianza kufungamana na Kitabu Kitakatifu cha Qur’an akiwa na umri wa miaka saba, na alianza kuhifadhi Qur’an katika madrasa ya kijiji chao.
Aliwahi kusimulia kuwa mara ya kwanza kusoma Qur’an hadharani ilikuwa katika hafla ndogo ya kijijini, ambako alitunukiwa zawadi ya qirsh ishirini na tano (kipimo kidogo cha fedha ya Kimisri) kama heshima ya usomaji wake.
Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Misri, alisema: "Ninapenda kusoma Qur’an kutokana na mapenzi yangu ya dhati kwa Kitabu hiki Kitukufu, bila tamaa ya umaarufu wala manufaa ya kidunia."
Safari yake ya Qur’an ilianza katika kijiji kidogo mkoani Dakahlia, lakini mafanikio makubwa yalijitokeza huko Kafr Suleiman Al-Bahri, katika kitovu cha Faraskur, mkoani Damietta.
Alieleza kuwa hiyo ilikuwa ni hatua ya mabadiliko katika maisha yake, akisema kuwa familia yake ilimhimizia kueneza sauti yake na usomaji wake kwa maeneo mengine mapana.
Baada ya muda si mrefu, jina lake likasikika kote mkoani Damietta, na haikuwahi kufanyika hafla yoyote au tukio lolote la kidini pasipo uwepo wake na sauti yake tukufu akisoma Qur’an.
Sikiliza baadhi ya qiraa zake hapa chini.
4284372