IQNA

Misri yaadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Qari mashuhuri Sheikh Mahmud Ali Al-Banna

21:15 - July 21, 2025
Habari ID: 3480978
IQNA – Taasisi ya Al-Azhar na Wizara ya Wakfu ya Misri zimemuenzi Sheikh Mahmud Ali Al-Banna, mmoja wa wasomaji wa Qur’ani mashuhuri wa karne ya 20, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo chake.

Kituo cha Kimataifa cha Al-Azhar cha Fatwa za Kielektroniki pamoja na Wizara ya Wakfu wametoa taarifa rasmi kuadhimisha miaka 39 tangu kifo cha Sheikh Al-Banna, aliyefariki dunia tarehe 20 Julai 1985.

 “Sheikh Al-Banna alikuwa nguzo kuu katika tasnia ya usomaji wa Qur’ani, akijulikana kwa mtindo wake wa kusoma kwa hisia na kwa heshima,” ilisema taarifa ya Al-Azhar, ikiongeza kuwa alikuwa “miongoni mwa maqari wa kipekee na mashuhuri nchini Misri na duniani kote.”

 Kituo hicho kilieleza kuwa Sheikh Al-Banna aliacha urithi mkubwa wa  usomaji wa Qur’ani na alianzisha mtindo wa kipekee wa usomaji. Alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Umoja wa Wasomaji wa Qur’ani wa Misri na alihudumu kama makamu mwenyekiti wake mwaka 1984.

“Mwenyezi Mungu amrehemu Sheikh Al-Banna na awabariki wote waliomsikiliza, popote walipo,” taarifa hiyo ilihitimisha kwa dua.

Wizara ya Wakfu pia ilimuenzi, ikimtaja kuwa “mfano wa nidhamu na kujitolea katika kuhudumia Qur’ani Tukufu.”

Sheikh Al-Banna alizaliwa mwaka 1926 na alifariki akiwa na umri wa miaka 59, baada ya miongo kadhaa ya mchango katika elimu ya Qur’ani na usomaji wa hadhara.

Wizara hiyo ilisisitiza kuwa aliingia mapema katika maisha ya kidini ya kitaifa, akijiunga na Redio ya Misri mwaka 1948 akiwa na umri wa miaka 22—na hivyo kuwa miongoni mwa makari wa kwanza waliopata leseni rasmi wakati huo.

 Taarifa hiyo ilieleza kuwa sauti yake “ilitambulika kwa utajiri wa maqamat, uhalisia wa hisia katika usomaji, na uwezo wa kipekee wa kugusa nyoyo za wasikilizaji.”

Sheikh Al-Banna alikuwa akiswalisha sala za Tarawehe katika misikiti mikubwa ya Misri kama vile Msikiti wa Al-Ahmadi huko Tanta na Msikiti wa Al-Hussein jijini Cairo. Pia aliwakilisha Misri katika mikutano ya kimataifa ya Qur’ani, sauti yake ikisikika katika maeneo matukufu kama vile Misikiti Miwili Mitakatifu, Msikiti wa Al-Aqsa, Msikiti wa Umawiyyah huko Damascus, na misikiti mbalimbali barani Ulaya na Asia.

 Wizara ilimtaja kuwa “alikuwa alama ya heshima, utaratibu, na kujitolea kwa Qur’ani Tukufu.”

 

3493920/

captcha