IQNA

Usomaji wa Qur’ani uliomfanya Sheikh al-Sayyid Saeed kupewa lakabu ya "Mfalme wa Maqari"

15:48 - May 25, 2025
Habari ID: 3480739
IQNA – Sheikh al-Sayyid Saeed, aliyefariki dunia Jumamosi, alijulikana kwa heshima kubwa kama “Sultan al-Qurra” (Mfalme wa Wasomaji wa Qur’an), kutokana na usomaji wake wa kipekee wa Qur’an.

Ni usomaji wake wa Surah Yusuf uliovutia nyoyo nyingi na ambao wengi wanauona kuwa ni kazi yake bora zaidi iliyowahi kurekodiwa.

Katikati ya miaka ya 1990, usomaji huu ulikuwa ukisikika kutoka kila nyumba, duka, na hata kwenye usafiri wa umma. Kanda za kaseti zilizosheheni usomaji huo ziliuzwa kwa wingi kila mahali.

Wengi wanaamini kuwa usomaji huu wa Surah Yusuf ndio uliokuwa hatua ya mabadiliko makubwa katika maisha ya Sheikh Saeed, na mafanikio haya makubwa ndiyo yaliyomletea umaarufu na kumpa lakabu au jina la "Sultan al-Qurra" ,  jina ambalo amebeba hadi mauti yake miongoni mwa wasomaji mashuhuri wa Misri.

Sheikh al-Sayyid Saeed alizaliwa tarehe 7 Machi, 1943, na alikulia katika mazingira ya Qur’ani Tukufu. Alikamilisha kuhifadhi Qur’ani yote kabla hajafikisha umri wa miaka saba, chini ya uangalizi wa Sheikh Abd al-Muhammed Osman katika madrasa ya kijiji chao.

Ingawa mwanzo wa shughuli zake za Qur’ani ulikuwa katika kijiji cha Dekhleya, jina lake lilianza kupata umaarufu zaidi katika mkoa wa Damietta, hususan katika eneo la Kafr Suleiman, ambapo alikuwa akisema: “Ni kijiji cha Damietta kilichoniita ‘Sheikh’ kwa mara ya kwanza, na huko ndiko nilijulikana kabla hata ya watu wa kwetu kunitambua.”

Baadaye, Sheikh Saeed alijiunga na duru ya maqari mashuhuri wa Misri na alishiriki katika hafla mbalimbali za Qur’ani, akiwasoma pamoja na wakongwe wa usomaji wa Qur’ani kama vile Sheikh Mohammed Sidiq Minshawi, Mustafa Ismail, Abdul Fattah al-Shashaai, Mahmoud Ali al-Banna, Abulainain Shuaisha, na maqari wengine maarufu wa Misri.

Aidha, alisoma Qur’ani katika mataifa mbalimbali, yakiwemo Iraq, Falme za Kiarabu (UAE), Lebanon, Iran, Uswisi, Afrika Kusini, na Jamhuri ya Azerbaijan.

Sheikh Saeed pia aliwafundisha wanafunzi wengi, baadhi yao wakiwa miongoni mwa kizazi kipya cha maqari wa Misri wanaoendeleza mtindo wake wa kusoma.

Sheikh al-Sayyid Saeed alifariki dunia tarehe 24 Mei, 2025, akiwa na umri wa miaka 82.

Ifuatayo ni Qiraa yake ya aya 19 hadi 31 za Surah Yusuf:

4284484

Kishikizo: qari misri
captcha