IQNA

Uwezo mkubwa wa Hamas wa kukabiliana na adui Mzayuni

16:56 - December 17, 2021
Habari ID: 3474686
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, sasa harakati hiyo ya Kiislamu ina nguvu kubwa za kijeshi ambazo zinaiwezesha kupiga popote katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.

Mahmoud al Zahar ameyasema hayo Jumatano na kuongeza kuwa, mazoezi ya jana ya kijeshi yanazidi kuthibitisha kwamba harakati ya HAMAS hivi sasa iko imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote na imejiwekea mikakati imara na madhubuti ya kuikomboa Quds.

Ikumbukwe kuwa Brigedi za Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeamua kufanya luteka na mazoezi ya kijeshi kwa jina la Ngao ya Quds ili kujiweka tayari kwa mapambano na kukabiliana na aina zote za mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza.

Brigedi hizo zinasisitiza kuwa, HAMAS itaendelea na muqawama na mapambano hadi zitakapokombolewa ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na kuheshimiwa matukufu ya wananchi wa Palestina. 

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Mahmoud al Zahar amesema, baraza jipya la mawaziri la adui Mzayuni linahaha kuvutia uungaji mkono wa ndani ya utawala wa kizayuni na ndio maana hivi sasa linataka kuonesha kuwa limechukua misimamo mikali zaidi ya kuwakandamiza Wapalestina.

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameongeza kuwa, zile nchi ambazo zimetangaza rasmi kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zitambue kwamba, utawala huo pandikizi hauna mwamana hata kidogo na hausiti hata kidogo kudhihirisha kinyama uadui wake kwa taifa lolote lile.

Jumanne ya tarehe 14 Disemba ilisadifiana na mwaka wa 34 tangu kuasisiwa Harakati ya Mapambano ya Kislamu ya Palestina HAMAS.

Harakati ya Hamas ilitangaza rasmi uwepo wake 1987. Hamas iliasisiwa na Sheikh Ahmed Yassin kutoka miongoni mwa vikosi vya Ikhwanul-Muslimin ya Palestina kwa kusambazwa hati yake 1988. Hati ya chama cha Hamas ilikuwa na viini vikuu vitatu kuhusiana na kadhia ya Palestina ambavyo ni: Wapalestina, Waarabu na Uislamu. Kwa maneno mengine ni kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilikuwa ikiamini kwamba, mbali na Wapalestina, mataifa ya Kiarabu na Kiisamu nayo yanapaswa kusaidia ukombozi wa Palestina kwani Palestina ni nchi ya Kiarabu na Kiislamu.

/4021405

captcha