Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, kundi hilo liliwahimiza Wapalestina kutoka maeneo yanayokaliwa kwa mabavu "kuhamasisha juhudi zote mwezi huu kwa kusafiri kwenda Msikiti wa Al-Aqsa, kubaki imara, na kukaa katika itikafu."
"Haya na yawe ni siku na nyusiku zenye baraka za Ramadhani kwa ajili ya ibada, na mapambano dhidi ya adui na makundi ya walowezi wa Kizayuni. Aidha Hamas imesema waumini wajitokeze kwa ajili ya kuulinda mji wa al-Quds na Msikiti wa Al-Aqsa hadi ukombozi kamili,
Harakati hiyo pia iliwataka Wapalestina kote ulimwenguni kuandaa "mipango na matukio ya mshikamano kwa wingi zaidi ili kuwaunga mkono ndugu zao huko Gaza, Ukingo wa Magharibi, na al-Quds."
Wakati huo huo, Ijumaa jioni, Sheikh Ekrima Sabri, mhubiri wa Msikiti wa Al-Aqsa, alisema utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukichukua hatua kali za ukandamizaji katika al-Quds inayokaliwa kwa mabavu. Alibainisha kuwa utawala wa Kizayuni unakusudia kupunguza idadi ya Wapalestina kwenye msikiti huo.
Kila mwaka wakati wa Ramadhani, utawala wa Kizayuni wa Israel huweka vikwazo vinavyoathiri uwezo wa Wapalestina kufikia Msikiti wa Al-Aqsa katika al-Quds Mashariki iliyokaliwa kwa mabavu.
Msikiti wa Al-Aqsa ni eneo la tatu takatifu zaidi katika Uislamu.
Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikalia al-Quds Mashariki, ikijumuisha Msikiti wa Al-Aqsa, wakati wa Vita vya Waarabu na Israel vya 1967 hatua ambayo haijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa.
Mnamo Julai mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliamua kuwa ukaliaji wa muda mrefu wa Israel wa maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria na ilitaka kuondolewa kwa vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi na al-Quds Mashariki.
3492092