Mwandishi huyu, ambaye ni mmoja wa wanazuoni wakuu wa Kisunni, katika kitabu hiki, nazungumzia maswali ya muda mrefu yanayohusu uongozi katika Uislamu pamoja na suala la umoja wa Waislamu.
Tukio la Ghadir Khum lilitokea 18 Dhu'l-Hijjah mwaka 10 Hijria (10 Machi 632 Miladia), muda mfupi kabla ya kufariki kwa Mtume (SAW), na limetajwa katika vyanzo vingi vya Kiislamu. Kwa mujibu wa riwaya za kihistoria, Mtume (SAW) alisimamisha msafara wake akiwa njiani kurejea kutoka katika Hija ya kuaga (Hajjatul-Widaʿ), kisha akawahutubia umati mkubwa wa Maswahaba.
Katika khutuba hiyo, alitamka kauli maarufu: “Yule ambaye kwamba mimi ni (Mawla) mwenye kumtawalia mambo yake, huyu Ali vile vile ni (Mawla) mwenye kumtawalia mambo yake. Ewe Allah, kuwa rafiki kwa yule ambaye ni rafiki, na uwe adui kwa yule ambaye ni adui kwake.”
Tamko hili limefasiriwa kwa namna mbalimbali. Waislamu wa Kishia wamekuwa wakiliona kama tamko la wazi la kumteua Ali bin Abi Talib (AS) kuwa Khalifa wa Mtume (SAW) baada ya yeye kuaga dunia.
Kwa upande mwingine, wanazuoni wa Kisunni wengi wamelitafsiri tamko hili kwa muktadha wa mapenzi, heshima, na uongozi wa kiroho , badala ya kuwa tangazo la uongozi wa kisiasa. Lakini kazi hii ya Sheikh Tahir-ul-Qadri inalenga kutumia vyanzo vya Kisunni pekee kuthibitisha tukio la Ghadir na kufungua mlango wa maelewano kati ya tafsiri hizi mbili.
Mjuwe Sheikh Muhammad Tahir-ul-Qadri
Muhammad Tahir-ul-Qadri ni mwanazuoni mashuhuri wa kimataifa kutoka Pakistan, mtaalamu wa sheria ya Kiislamu, na mwanzilishi wa taasisi ya kimataifa ya 'Minhaj-ul-Qur’an International' inayojishughulisha na elimu ya Kiislamu. Anaheshimika sana katika nyanja za kielimu na za kidini, na anajulikana kwa kazi zake katika kupambana na misimamo mikali pamoja na uandishi kuhusu katiba katika Uislamu.
Akiwa na mafunzo ya kitamaduni ya Kiislamu sambamba na elimu ya vyuo vya Kimagharibi, Sheikh Qadri ameandika zaidi ya vitabu 500 kwa Kiarabu, Kiurdu na Kiingereza. Tamko la Ghadir ni mojawapo ya juhudi zake katika kukuza umoja wa kifikra wa Kiislamu kwa njia ya utafiti wa kielimu.
Yaliyomo
Katika kitabu hiki cha Tamko la Ghadir, Sheikh Qadri anawasilisha uchambuzi kina na wa kitaalamu kuhusu khutuba ya Ghadir, akibainisha uzito wa kimaarifa na kimaadili wa tukio hilo ndani ya mtazamo wa Kisunni. Kauli kuu ya kitabu ni kuwa tamko la Mtume (SAW) linaashiria uongozi ulioongozwa na Wahyi, hata kama haukuwasilishwa kwa istilahi ya kisiasa.
Kitabu hiki kinajivunia kutumia vyanzo vya hadithi sahihi za Kisunni, maoni ya mafaqihi wa Kisunni, na tafsiri za wanazuoni wa zamani.
Katika dibaji ya kitabu, Sheikh Qadri anaandika: “Leo ni tarehe 18 Dhul-Hijjah, siku ambayo Mtume (SAW) alisimama Ghadir Khumm alipokuwa akirejea kutoka Hajjatul-Widaʿ kwenda Madina, na akiwa amezungukwa na Maswahaba (RA), alinyanyua mkono wa Ali al-Murtadha (AS) na kutangaza: ‘Yule ambaye kwamba mimi ni (Mawla) mwenye kumtawalia mambo yake, huyu Ali vile vile ni (Mawla) mwenye kumtawalia mambo yake’
Anaendelea: “Hili lilikuwa ni tamko la mamlaka ya kiroho ya Ali, na kukubali bila masharti tamko hilo ni wajibu kwa waumini hadi Siku ya Kiyama. Kukataa mamlaka hii ya kiroho ni sawa na kumkataa Mtume mwenyewe. Mwandishi mnyenyekevu wa kazi hii ameona kuwa baadhi ya watu wanakataa ukweli huu aidha kwa kutojua au kwa chuki, jambo linalozua mgawanyiko usio wa lazima katika umma wa Kiislamu.”
Katika sehemu nyingine ya dibaji, Sheikh Tahir-ul-Qadri anaeleza: “Kiini cha mjadala ni kwamba tamko la Mtume (SAW) katika Ghadir Khumm lilithibitisha kwamba mamlaka ya kiroho ya Ali ni mwendelezo wa mamlaka ya kiroho ya Mtume Muhammad (SAW). Ingawa mlango wa Unabii umefungwa baada ya Mtume (SAW), Mwenyezi Mungu alifungua njia mpya za kuendeleza baraka za Mtume hadi Siku ya Kiyama. Baadhi ya njia hizi zilikuwa wazi, nyingine za ndani. Njia ya ndani ilikuwa ni uongozi wa kiroho, na Ali al-Murtadha (AS) ndiye aliyekuwa wa kwanza kushika nafasi hiyo.”
“Baada ya hapo, mnyororo huu wa uongozi uliendelea kwa kizazi chake, hadi kwa Maimamu kumi na wawili. Katika kipindi hicho, viongozi wengi walitokea katika anga ya kiroho, lakini wote , moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, walikiri utiifu wao kwa Ali (AS). Hakuna aliyepinga nasaba hiyo. Na mnyororo huu utaendelea hadi Siku ya Kiyama, hadi atakapodhihiri Imamu wa mwisho , Imamu Muhammad al-Mahdi (AS), ambaye ndiye Imamu wa kumi na mbili na Khalifa wa mwisho. Kwa kupitia kwake, njia zilizo wazi na zilizofichika zitaunganishwa tena; yeye atakuwa mrithi wa kiroho na kisiasa. Mtu yeyote atakayemkataa Imamu Mahdi (AS) basi amekataa dini kwa sura zake zote mbili , ya ndani na ya nje.”
Wito wa Umoja
Kitabu hiki kimekusanya riwaya hamsini) kuthibitisha tukio la Ghadir na kubainisha maneno ya Mtume Muhammad (SAW) pamoja na sifa tukufu za Imam Ali (AS).
Mwandishi ameweka msingi wa mjadala huu katika vyanzo vya Kisunni ili kuwatia moyo wasomaji kutoka madhehebu mbalimbali za Kiislamu kuangalia kwa kina na kwa heshima urithi wa Ghadir Khumm.
Mmoja wa wasomaji wa Amazon, aitwaye Iqbal, aliandika maoni yake kuhusu kitabu hicho mnamo Machi 2013: “Ni jambo la kushangaza kuona jinsi Imamu Ali (Khalifa wa nne katika Uislamu) anavyoheshimiwa na kupendwa kwa ushahidi wa hadithi za Mtume (SAW) kutoka katika vitabu visivyo vya Kishia.” Akaongeza: “Kitabu hiki kimeongeza mapenzi yangu kwa Imam Ali.”
3493403