IQNA

Mufti wa Quds alaani Wazayuni waliouvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa

13:06 - December 17, 2020
Habari ID: 3473464
TEHRAN (IQNA) – Mufti wa Quds (Jerusalem) amelaani vikali hatua ya Walowezi wa Kizayuni kuuhujumu Msikiti wa Al Aqsa mjini humo na kuweka nembo ya Kiyahudi ya Menorah katika msikiti huo.

Katika taarifa, Sheikh Mohamad Hussein, Mufti Mkuu wa Quds na Ardhi za Palestina ametoa taarifa na  kulaani hujuma  ya  walowezi wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa, kwa kisingizio cha kutekeleza ibada za Kiyahudi, ambapo walifika mbele ya msikiti huo na kuweka nembo ya Kiyahudi ya Menorah katika mlango wa msiki huo na hivyo kuuvunjia heshima.

Katika taarifa hiyo aidha Sheikh Hussein amelaani kitendo cha Wazayuin kuharibu  makaburi ya mashahidi katika eneo la kaskazini la Makaburi ya Al Yusufiya katika upande wa Babul Absat mjini Quds. Amesema kitendo hicho ni katika njama za kuangamiza makaburi ya Waislamu na kubadilisha eneo hilo kuwa bustani ya Mayahudi.

Mufti wa Quds amesema hujuma hiyo ni sehemu ya njama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya matukufu ya Kiislamu.

Kiongozi huyo wa Kiislamu Palestina ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua ya kuuzuia utawala wa Kizayuni kuendeleza hujuma hizo dhidi ya matukufu wa Kiislamu.

Asubuhi ya Jumatatu wiki hii, walowezi wa Kizayuni waliokadiriwa kuwa 145 waliuhujumu Msikiti wa Al Aqsa kwa lengo la kuadhimisha siku kuu ya Kiyahudi inayojulikana Hanukkah, au "Sikukuu ya Wamakabayo". Uvamizi huo ulitekelezwa kwa himaya kamili ya askari wa utawala dhalimu wa Israel.

Katika hujuma hiyo, Wazayuni walijaribu kuingiza msikiti humo nembo kuu ya Uyahudi yenye mishumaa saba ambayo inajulikana kama Menorah.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umekuwa ukiandamwa na njama mtawalia za utawala vamizi wa Israel, hatua ambazo zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

3941636

captcha