IQNA

Maandamano makubwa zaidi ya Uholanzi katika miongo miwili, ni ya watetezi wa Palestina

17:06 - May 19, 2025
Habari ID: 3480704
IQNA – Mji wa The Hague, Uholanzi umeshuhudia maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina na Gaza siku ya Jumapili.

Maelfu kwa maelfu ya waandamanaji waliovaa nguo nyekundu walitembea barabarani mjini The Hague wakitaka serikali ichukue hatua ya kusitisha vita vya kinyama vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Waandaaji wa maandamano hayo walisema ni maandamano makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha miaka ishirini, ambapo mashirika ya haki za binadamu na misaada, yakiwemo Amnesty International, Save the Children na Madaktari Wasio na Mipaka , walikadiria idadi ya watu waliohudhuria kuwa zaidi ya 100,000.

Mitaa ya mji mkuu wa kisiasa wa Uholanzi ilikuwa imejaa watu wa rika zote — wazee, vijana, na hata baadhi ya watoto wachanga waliokuwa kwenye maandamano yao ya kwanza.

“Tuna matumaini kuwa hili ni pigo la kengele kwa serikali,” alisema mwalimu Roos Lingbeek, aliyekuwa ameambatana na mumewe na binti yao mchanga wa wiki 12, Dido, aliyekuwa amelala kwenye bega la mama yake huku wazazi wake wakiwa na bango lililoandikwa kwa maneno mafupi: “STOP.”

Maandamano hayo yalipitia kwenye Jumba la Amani, makao makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya Umoja wa Mataifa, ambapo mwaka jana majaji waliiagiza Israel kuchukua hatua zote kuzuia vifo, uharibifu na vitendo vyovyote vya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Waandamanaji walitembea umbali wa kilomita 5 kuzunguka katikati ya jiji la The Hague, kwa lengo la kuunda mstari mwekundu huku  wakisema serikali imeshindwa kuweka mpaka huo.

“Tunatoa wito kwa serikali ya Uholanzi: isitishe msaada wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi kwa Israel maadamu utawala huo unaendelea kuzuia misaada ya kibinadamu na wakati huo huo inatenda mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu katika Gaza na Maeneo Yaliyokaliwa ya Palestina,” alisema Marjon Rozema kutoka Amnesty International.

Sera ya Uholanzi kuhusu Israel ni mojawapo ya masuala mengi yanayosababisha mgawanyiko katika serikali ya muungano dhaifu ya nchi hiyo. Kiongozi mkali wa mrengo wa kulia Geert Wilders ni muungaji mkono mkubwa wa Israel, na chama chake cha kupinga wahamiaji, Party for Freedom, ndicho kinachoongoza kwa idadi ya viti katika bunge la nchi hiyo.

Wiki iliyopita, waziri wa mambo ya nje Caspar Veldkamp kutoka chama cha kati-kulia cha VVD aliitaka Umoja wa Ulaya kuchunguza upya makubaliano ya kibiashara na Israel, akidai kuwa kuzuiwa kwa misaada ya kibinadamu kunakiuka sheria za kimataifa. Wilders alijibu kwa hasira, akisema mwito huo ni “matusi kwa sera ya baraza la mawaziri.”

3493149

Kishikizo: uholanzi palestina
captcha