IQNA

Mkutano wa Qur’ani ya Nukta Nundu (Braille) Kashmir wajadili msaada kwa wenye ulemavu wa macho

15:23 - August 19, 2025
Habari ID: 3481106
IQNA – Jumapili, mji wa Banihal katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na India uliandaa Mkutano wa Pili wa Qur’ani ya Braille kwa watu wenye ulemavu wa kuona.

Mkutano huo uliwaleta washiriki kutoka India nzima na nje ya nchi, huku wazungumzaji wakisisitiza elimu, teknolojia na masomo ya kidini kama nyenzo muhimu za kuwawezesha walemavu wa kuona.

Mkutano uliongozwa na Moulana Haji Muhammad Hussain Abdul Qadir Mirchi, raia wa Afrika Kusini mwenye asili ya India, ambaye anaendesha shule ya kipekee kwa walemavu wa kuona nchini Afrika Kusini. Taasisi hiyo inatoa elimu na mafunzo ya sayansi za kisasa na teknolojia kwa wanafunzi kutoka zaidi ya nchi 35.

Hafla hiyo iliandaliwa kwa pamoja na Jumuiya ya Walemavu ya Jammu na Kashmir (Srinagar), Madrasa Noorul Qur’an ya Maharashtra, na Darul Uloom Noomaniya Banihal. Malengo yake yalikuwa kuwawezesha takribani watu 70,000 wenye ulemavu wa kuona katika Jammu na Kashmir kupitia elimu, mafunzo na masomo ya dini kwa kutumia maandishi ya Braille.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Moulana Farid Selia kutoka Madrasa Noorul Qur’an, Maharashtra, alisema kuwa idadi ya watu wenye ulemavu wa kuona katika Jammu imeongezeka kutoka 58,000 mwaka 2011 hadi kufikia 70,000 leo.
“Wengi wao wamefungwa majumbani bila elimu wala ajira. Wazazi wanapaswa kuchukua hatua na kuwapeleka watoto wao kwenye taasisi kama Darul Uloom Noomaniya ili wapate fursa za maendeleo,” alisema.

Moulana Muhammad Sajad Nadvi wa Jamia Riyaz-ul-Soliheen, Sopore, alisifu juhudi za Mufti Zulfiqar Ahmad, msimamizi wa Darul Uloom Noomaniya Banihal, kwa kuanzisha elimu ya Qur’ani kwa njia ya Braille katika J&K.
Alibainisha kuwa ingawa kuna taasisi nyingi zinazofanya kazi kwa ajili ya walemavu, jitihada za kukuza elimu ya Qur’ani kupitia  Nukta Nundu au Braille bado ni chache Kashmir.

Mkutano pia ulimshirikisha Muhammad Saqib, kijana mwenye ulemavu wa kuona kutoka Bihar ambaye kwa sasa anasomea Maharashtra. Akiwa ni msahihishaji wa Qur’ani ya  Nukta Nundu, alionyesha jinsi elimu ilivyobadilisha maisha yake kwa kuonesha ujuzi wake katika zana za kidigitali, teknolojia ya habari na akili mnemba (AI). “AI imerahisisha maisha yetu, ikituwezesha kusimama bega kwa bega na jamii,” alisema.

Katika hotuba yake, Mirchi alitoa wito wa mshikamano kati ya serikali na jamii ya kiraia kusaidia walemavu wa kuona, akieleza jukumu hilo kuwa “gumu na lenye changamoto.”
Alisema kusaidia watu wasioona ni jukumu la kimaadili na kidini. “Amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ni kwamba tuwasaidie kwa kadri ya uwezo wetu, iwe binafsi au kupitia mashirika, kwani jamii imesahau watu hawa,” aliongeza.

Alionyesha pia jinsi teknolojia ya habari na akili mnemba zilivyofungua njia mpya kwa walemavu wa kuona, zikiwarahisishia maisha na kuwapa heshima katika hatua za maendeleo.

Zaidi ya watu 100 wenye ulemavu wa kuona, wengi wao kutoka Jammu na Kashmir, walihudhuria mkutano huo. Mbunge wa Banihal, Haji Sajjad Shaheen, ambaye pia alikuwepo, alisema ameguswa sana na ujasiri na uwezo wa washiriki. Alitangaza kutoa rupia lakh 2 (takribani milioni 2 Tsh) kutoka mfuko wake wa maendeleo ya jimbo kwa ajili ya kununua vifaa vya kielimu vya kisasa kwa wanafunzi wasioona.

Wazungumzaji kadhaa walisisitiza kuwa wazazi hawapaswi kuendelea kuwaona watoto wasioona kama mzigo, wakibainisha kwamba kwa elimu na mafunzo sahihi wanaweza kufanikisha mambo makubwa. Washiriki walionyesha uwezo wao wa kusoma vitabu vya  Nukta Nundu, kutumia kompyuta na simu janja au smartphone, pamoja na teknolojia ya kisasa ikiwemo akili bandia.

Katika hotuba yake ya kufunga, Mufti Zulfiqar Ahmad aliwahimiza wazazi kuwasomesha watoto wao si tu katika elimu ya Qur’ani, bali pia masomo ya kisasa kama sayansi na hisabati. Alisema kuwa mkutano huu ni hatua muhimu katika kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona.

Hafla hiyo pia ilimshirikisha Irfan Ahmad, mchezaji wa michezo ya walemavu na mchezaji wa kriketi kutoka Pampore, ambaye ameiwakilisha Jammu na Kashmir katika mashindano ya taifa ya kriketi kwa walemavu wa kuona tangu mwaka 2015. Alieleza mitazamo mibaya inayowakabili watu wasioona nchini India na akawashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono bila masharti.

Mkutano ulimalizika kwa ujumbe mzito kwamba walemavu wa kuona si mzigo, bali ni rasilimali kwa jamii, na wana uwezo wa kujitegemea na kufanikisha mambo makubwa kupitia elimu na teknolojia.

 

3494294

captcha