Akizungumza kupitia hotuba ya televisheni iliyotangazwa kutoka mji mkuu wa Lebanon, Beirut, jioni ya Jumatano, Sheikh Naim Qassem alitaja shambulizi hilo la anga kuwa ni hujuma ya pamoja ya Marekani na utawala wa Kizayuni, na sehemu ya mpango wa “Israel Kubwa”.
Neno “Israel Kubwa” limekuwa likitumika tangu Vita vya Waarabu na Israel vya mwaka 1967, likiashiria maeneo yaliyokaliwa na Israel, yakiwemo Mashariki mwa al-Quds, Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza, Rasi ya Sinai ya Misri, na Milima ya Golan ya Syria. Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Israel aliashiria tena mpango huo na kusema analenga kunyakua eneo kubwa kutoka Mto Nile nchini Misri hadi Mto Furat nchini Iraq kama sehemu ya mpango wa 'Israel Kubwa'.
“Ujumbe wa mashambulizi ya utawala wa kibeberu dhidi ya viongozi wa Hamas walioko Qatar ni hatari sana. Sisi kama Waislamu hatupaswi kukaa kimya. Tunasimama na Qatar katika kukabiliana na ukatili huu usio na mfano. Hili ni sehemu ya mpango wa ‘Israel Kubwa’,” alisema Sheikh Qassem.
“Uvamizi dhidi ya Qatar ulipangwa kwa pamoja na Marekani na Israel, na ulitekelezwa kwa idhini ya Washington,” aliongeza.
Alieleza kuwa suala la Palestina ni “jambo kuu na la msingi” kwa ulimwengu wa Kiislamu, huku akipipongza tukio la hivi karibuni la kulipiza kisasi karibu na al-Quds iliyokaliwa kuwa ni kitendo cha ujasiri na ushujaa.
Alisisitiza kuwa Hizbullah kwa muda mrefu imekuwa ikizuia kutimia kwa dhana ya “Israel Kubwa”, akieleza kuwa harakati hiyo ya Muqawama au mapambano ya Kiislamu ndiyo kikundi pekee cha kijeshi nchini Lebanon chenye uwezo wa kukabiliana na uchokozi wa Israel.
Sheikh Qassem pia alikataa wito wa kuitaka Hizbullah iweke chini silaha zake, akisema kuwa wanaounga mkono wito huo ni watu waliopoteza mwelekeo.
“Harakati ya Muqawama imejitoa Muhanga katika kulinda Lebanon, hasa viongozi wake waliouawa shahidi katika mashambulizi ya Israel ambao ni Sayyed Hassan Nasrallah na Sayyed Hashem Safieddine. Hizbullah na imezuia njama za adui wa Kizayuni na haikuruhusu kuikalia ardhi ya Lebanon,” alisema.
3494559