IQNA

Mafundisho ya Qur’ani yadhihirika kwa kina katika Mashairi ya Rumi, asema mwanazuoni

16:37 - September 30, 2025
Habari ID: 3481305
IQNA – Mwanazuoni kutoka Iran, Karim Zamani, asema kazi za Rumi, hasa Masnavi, zinaakisi kwa kina mafundisho ya Qur’ani Tukufu, kuanzia misingi ya itikadi hadi mtindo wa simulizi.

Jalal al-Din Rumi (1207–1273 M), mshairi, malenga na sufi wa Kiajemi ambaye urithi wake umeenea katika tamaduni na karne nyingi, bado ni miongoni mwa washairi wanaosomwa sana duniani. Kitabu chake cha Masnavi-ye Ma’navi mara nyingi huchukuliwa kama tafsiri ya kiroho ya Qur’ani, jambo ambalo wataalamu huendelea kusisitiza.

Katika mazungumzo ya hivi karibuni na IQNA, Karim Zamani alieleza kwa kina kipengele hiki cha kazi za Rumi. “Rumi ameakisi mafundisho ya Qur’ani kwa ustadi mkubwa,” alisema. “Kuanzia tauhidi ya Mwenyezi Mungu hadi matendo ya mwanaadamu, athari zake, na masuala mengine ya kiroho, maandiko yake yanabeba hekima ya Qur’ani.”

Kwa mujibu wa Zamani, ambaye ameandika kitabu maarufu cha maelezo juu ya Masnavi, matumizi ya Rumi ya hadithi na mifano yanafanana na mbinu ya Qur’ani katika kufundisha.

“Hata katika mtindo wa simulizi, anafuata njia ya Qur’ani,” alifafanua. “Rumi hasimuli hadithi kwa ajili ya burudani tu, wala hatumii mifano kwa ajili ya kuchekesha. Lengo lake ni kuongoza, kuamsha tafakuri, kama Qur’ani inavyosema: ‘Tunawapigia watu mifano ili wapate kutafakari.’” (Surah al-Hashr, aya ya 21)

Zamani, ambaye amejikita sana katika tafsiri ya Qur’ani na masomo ya Rumi, alisisitiza kuwa muunganiko huu ndio sababu ya ushawishi wa kudumu wa mshairi huyo. “Kioo cha maisha ya Rumi kilikuwa ni ukweli wake,” alisema. “Alizungumza kama alivyokuwa akiishi, na ndiyo maana maneno yake yana nguvu hadi leo.”

Maandishi ya Rumi kwa muda mrefu yamejulikana kwa kuchanganya athari kutoka tamaduni mbalimbali. Zamani alitaja kuwa kuna athari za falsafa ya Platoni, Neoplatonism, Gnosticism ya Kikristo, teolojia ya Kiislamu, na mafundisho ya washairi wa Kiajemi waliomtangulia kama Sana’i na Attar.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa mafanikio ya Rumi hayakuwa katika kuunganisha vipande vya fikra za wengine. “Aliyeyusha msukumo huo ndani ya tajiriba zake za kiroho na fikra zake binafsi,” alisema Zamani. “Kilichozaliwa kilikuwa ni kitu cha kipekee, kisicho na mfano wa kilichotangulia.”

“Kazi ya Rumi si mkusanyiko wa mawazo,” aliongeza. “Ni kama waridi linalochukua lishe kutoka kwenye udongo, maji, na mwangaza wa jua, lakini linatoa harufu ya kipekee isiyofanana na nyingine.”

Mwanazuoni huyo pia alitafakari kuhusu umuhimu wa Rumi katika zama hizi, akisema mwito wake wa upendo, huruma, na kiroho hauzuiliwi na mipaka ya kijiografia.

“Kwa mtazamo mmoja, mafundisho yake ni ya wanadamu wote, yakiwaongoza kuelekea ubinadamu wa kweli,” alisema Zamani. “Kwa mtazamo mwingine, ni sehemu ya urithi wetu wa kitaifa na kitamaduni, yakionyesha kuwa nasi pia tumetoa mchango mkubwa katika utamaduni wa dunia.”

3494809

captcha