“Nilikubali Uislamu mwezi Aprili mwaka 2021. Familia yangu ilishangaa lakini pia walinielewa. Nilichagua Msikiti wa Hagia Sophia mjini Istanbul kutangaza rasmi kusilimu kwangu. Uislamu umebadili maisha yangu kwa njia bora kabisa,” alisema Lyudmila, akisimulia jinsi ugonjwa wa saratani ulimfikisha kitandani karibu na mauti, kabla ya uponyaji wa kimiujiza uliomfungulia mlango wa hidaya.
Lyudmila alieleza kuwa madaktari walimwambia kuwa alikuwa na miezi miwili tu ya kuishi baada ya saratani kusambaa mwilini kote. Alikumbuka jinsi alivyopokea habari hizo kwa kusema: “Nitaishi,” akieleza kuwa imani yake kwa Mwenyezi Mungu, na pia msaada wa familia yake, vilikuwa nguzo kuu katika kipindi hicho kigumu.
“Ugonjwa huu ulinifundisha mambo mengi na kunisafisha kiroho. Nilipofanikiwa kuvuka mitihani hii, nilitambua kuwa jambo muhimu zaidi ni nguvu ya imani. Na hili ndilo ninalojitahidi kumwaambia kila mgonjwa ninaekutana naye – imani ndio msingi wa kila kitu.”
Baada ya kupona, Lyudmila alisilimu na kugeuza maumivu yake kuwa chemchemi ya huruma kupitia mradi wa misaada nchini Senegal. Hapo ndipo alipoanzisha Mila for Africa Foundation, inayowalenga hasa makundi mawili yaliyo katika hali ngumu barani Afrika: wagonjwa wa saratani na watu wenye ulemavu wa ngozi ambao ni maarufu kama albino.
Kupitia taasisi hiyo, Lyudmila hutoa msaada wa matibabu na ushauri wa kisaikolojia kwa watoto hao, sambamba na juhudi za kutoa elimu ya uelewa katika jamii ili kupunguza dhuluma na unyanyapaa.
Aidha, anajitahidi kuwaunganisha watoto hawa na elimu rasmi ili kuwaepusha na upweke na kutengwa. Hata hivyo, anasisitiza kuwa kubadilisha fikra za jamii ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji msaada wa vyombo vya habari na wafadhili ili sauti za waathirika zisikike.
Alimalizia kwa ushauri wenye uzito: “Muamini Mwenyezi Mungu, fanyeni huruma, na toeni msaada; kwa sababu kupitia matendo mema na kuwasaidia walioko katika haja, ndipo tunaweza kuubadilisha ulimwengu huu kwa pamoja.”
3493808