IQNA

Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai yapokea zaidi ya maombi 5,600 kwa toleo la 2026

21:07 - July 23, 2025
Habari ID: 3480988
IQNA – Toleo la 28 la Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai limevutia maombi 5,618 kutoka nchi 105, ikiwa ni idadi ya juu zaidi hadi sasa, ambapo asilimia 30 ya waliowasilisha maombi ni wanawake.

Waandalizi wa Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai (DIHQA) wametangaza ongezeko kubwa la ushiriki kwa toleo la 2026, wakipokea maombi kutoka kwa wahifadhi wa Qur’ani kutoka mataifa 105 duniani kote, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kwa mara ya kwanza, wanawake wamepewa kundi maalumu la kushiriki, na wameshiriki kwa asilimia 30 ya jumla ya waombaji.

Maombi yalifunguliwa kuanzia Mei 21 hadi Julai 20. Awamu ya awali ya tathmini ilianza mapema Julai na itaendelea hadi mwishoni mwa mwezi. Washiriki watakaofaulu hatua hii wataingia duru ya pili mwezi Septemba, ambapo tathmini zitafanywa kwa njia ya mtandao mbele ya majaji maalumu.

Wafinalisti wanatarajiwa kushiriki mashindanoni ana kwa ana wiki ya pili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka 1447 Hijria, mjini Dubai.

Bwana Ibrahim Jassim Al Mansouri, kaimu mkurugenzi wa DIHQA, alisema kuwa nchi iliyowasilisha maombi mengi zaidi ni Misri (1,410), ikifuatiwa na Pakistan, Indonesia, India, na Morocco. Pia maombi yalipokelewa kutoka kwa jamii za Waislamu katika Marekani, Kanada, Urusi, na nchi kadhaa za Ulaya, pamoja na mataifa ya Asia, Afrika, na Oceania.

Toleo hili limeleta mabadiliko ya kimfumo ili kuongeza ushiriki wa kimataifa. Haya ni pamoja na kuruhusu maombi ya moja kwa moja kutoka kwa watu binafsi, sambamba na uteuzi kutoka vituo vya Kiislamu vilivyotambuliwa au taasisi rasmi. Jumla ya zawadi sasa imepita Dirham milioni 12, ambapo washindi wa kwanza upande wa wanaume na wanawake watapata dola milioni moja kila mmoja.

Maafisa wamesema kuwa muundo huu mpya ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kukuza ushawishi wa tuzo hii, na kuhamasisha ushiriki wa kina katika Qur’ani kupitia kuhifadhi, kusoma kwa tartil, na kuelewa maana zake tukufu.

3493959/

captcha