IQNA

Wahifadhi Qur'ani kutoka Nchi 85 wajisajili katika Mashindano ya Qur’ani ya Dubai

23:53 - June 25, 2025
Habari ID: 3480858
IQNA – Wahifadhi Qur’ani kutoka nchi 85 wamesajili majina yao ili kushiriki katika toleo la 28 la Tuzo la Kimataifa la Qur’ani Tukufu la Dubai.

 

Tuzo hiyo ilitangaza kuwa usajili kwa toleo lake la 28 la kimataifa, la  mwaka  wa 2026, umeshuhudia idadi kubwa ya waliojitokeza ndani ya wiki tatu tu baada ya kuzinduliwa.

Ahmed Darwish Al Muhairi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kiislamu na Shughuli za Hisani huko Dubai na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo hiyo, alifichua kwamba idadi ya waliotuma maombi imepita wahifadhi 3,400 wa kuhifadhi Qur'ani kutoka nchi 85 duniani kote - na hivyo kuthibitisha sifa kubwa ya Tuzo hiyo na hamu ya kushiriki.

Alibainisha kuwa takwimu hii, ongezeko kubwa ikilinganishwa na matoleo ya awali, inaonyesha dira ya Tuzo ya kupanua ushiriki wa kimataifa na kupanua shughuli zake na kufikia kimataifa. Kwa mara ya kwanza, Tuzo hii imefungua ushiriki wa wanawake kupitia kitengo maalum na imeruhusu uteuzi wa moja kwa moja wa watu binafsi, pamoja na uteuzi wa kawaida wa nchi ya mshiriki au kituo cha Kiislamu kilichoidhinishwa.

Amesisitiza kuwa, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa ufadhili na uungaji mkono wa Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Imarati na Mtawala wa Dubai, Tuzo ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Dubai itaendelea kuimarisha hadhi yake ya kuwa tuzo kubwa zaidi na adhimu ya kuwaenzi wahifadhi Qur'ani.

Tuzo ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Dubai imetangaza dira mpya ya maendeleo kwa toleo lake la 28 katika mwaka wa (1447 AH - 2026 AD), ikilenga kuifanya iwe ya kipekee .

Thamani ya jumla ya zawadi ya Tuzo ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Dubai imeongezwa hadi zaidi ya AED 12 milioni. Mshindi wa kwanza katika kategoria za wanaume na wanawake atapata dola za kimarekani milioni moja, na zawadi ya kundi la Shakhsia wa Kiislamu wa Mwaka pia imepandishwa hadi dola milioni moja,

Miongoni mwa nyongeza muhimu katika toleo hili ni kujumuishwa kwa kategoria mahususi kwa wahifadhi wa Qur'ani wa kike, na kuinua jumla ya kategoria za tuzo hadi tatu: kuhifadhi Qur'ani kamili kwa wanaume, kuhifadhi Qur'ani kamili kwa wanawake, na tuzo ya Shakhsia ya Kiislamu ya Mwaka.

 

captcha