IQNA

Rais wa Iran asisitiza kujitokeza wananchi katika Siku ya Kimataifa ya Quds

8:05 - March 27, 2025
Habari ID: 3480446
IQNA-Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito kwa wananchi wa Iran kuonyesha umoja na mshikamano wao wakati wa Siku ya Kimataifa ya Quds, akisisitiza kwamba kujitokeza kwa wingi wananchi katika siku hii kutaonyesha msaada usiotetereka wa Jamhuri ya Kiislamu kwa malengo ya ukombozi wa Palestina.

Akizungumza Jumatano katika mkutano wa Baraza la Mawaziri, Rais Pezeshkian ameelezea matumaini yake kuwa wananchi wa Iran watajitokeza kwa wingi katika maandamano ya siku ya kimataifa ya Quds Ijumaa hii.

Siku ya Kimataifa ya Quds, iliyoanzishwa na muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini, huadhimishwa kila mwaka katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtakatifu wa Ramadhani. Siku hii adhimu ni jukwaa la kimataifa kwa Waislamu na wapenda uhuru kote duniani kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina na kuulani utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kutenda jinai dhidi ya Wapalestina.

Wakati huo huo Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu imetoa taarifa, ikiyahimiza mataifa yote huru, hasa Waislamu, kushiriki kwa nguvu katika matukio ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Taarifa hiyo imesisitiza umuhimu wa siku hii na kuitaja kuwa nembo ya Muqawama au mapambano dhidi ya dhuluma za kimataifa, ikiwa ni pamoja na ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Asia Magharibi.

Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Esmaeil Qa’ani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), pia amesisitiza kwamba Iran inajitolea kikamilifu kwa ajili ya malengo matukufu ya uhuru wa Palestina kutoka kwa uvamizi na ukatili wa Israel.

Akizungumza wakati wa kipindi cha "Minbar al-Quds," ambacho kimejumuisha hotuba za viongozi kadhaa wa Muqawama kwa heshima ya Siku ya Kimataifa ya Quds, Jenerali Qa’ani amesisitiza kuendelea msaada wa Jamhuri ya Kiislamu kwa taifa la Palestina kupitia msaada wa moja kwa moja kwa vikosi vya Muqawama na operesheni za kijeshi kama "Ahadi ya Kweli."

Aidha amesisitiza kwamba Iran itaendelea kuunga mkono Palestina "hadi lengo la mwisho la kukombolewa al-Quds (Jerusalem) litakapofikiwa."

Inafaa kuashiria hapa kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa urithi wa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Ammrehemu), ambaye anaheshimiwa kama kiongozi wa kiroho na Waislamu duniani kote. 

Mnamo mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalimpindua mtawala wa kiimla, Shah, aliyeungwa mkono na Marekani pamoja na Israel, Imam Khomeini aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa Quds ili Waislamu na wapenda haki kote duniani waweze kujitokeza katika siku hiyo katika maandamano na mijumuiko ya kuunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina sambamba na kulaani utawala wa Kizayuni wa Israel unaozikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Mji wa al-Quds (Jerusalem) unachukuliwa kuwa nembo ya ukombozi wa Palestina kwani unatazamiwa kuwa mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.

4273777

Habari zinazohusiana
captcha