
Katika ujumbe alioutuma kwa hafla iliyofanyika Kashmar, kaskazini mashariki mwa Iran, Ijumaa, kwa heshima ya wahifadhi wa Qur’ani Tukufu katika Mashindano ya Kitaifa ya Qur’ani yajulikanayo kama Tarannum Wahyi, Rais Pezeshkian alisisitiza nafasi ya pekee ya mahafidh na maqari wa Qur’ani. Mashindano hayo yaliandaliwa na Taasisi ya Kitaifa ya Mahd Qur’an.
Rais alisema: “Zaidi ya kusomwa, aya za Qur’an ni mwaliko wa tafakuri ya ndani na mfumo wa mwanga wa hekima unaoweza kuangaza maisha na tabia zetu.”
Akaongeza: “Katika mchakato huu wa mabadiliko, nyinyi wasomaji Qur'ani mna jukumu lisilo na kifani la kuhamisha nuru ya Qur’ani kutoka kurasa za kitabu hadi katika maisha ya kijamii na kuifanya ionekane zaidi katika jamii.”
Rais Pezeshkian alitaja tukio hilo la Qur’ani kuwa ni “dhihirisho la azma yenu kama walimu na walinzi wa Qur’ani, kundi lililokusanyika si kwa kusikiliza au kusherehekea tu, bali kuonyesha nguvu halisi ya Qur’ani katika maisha na kutimiza jukumu la kupeleka mwanga wa wahyi katika nyoyo na tabia.”
Aidha, alikumbusha maneno ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye mara kwa mara amesisitiza umuhimu wa kufahamiana na Qur’ani na athari za mafundisho yake katika maisha ya kila siku. Alisema: “Uwepo wenu unapaswa kufanya mifano hii yenye mwanga kuwa halisi katika jamii.”
Kwa matumaini, Rais alihitimisha: “Kukusanyika huku kwa baraka za Mwenyezi Mungu kiwe mwanzo wa sura mpya — sura ambayo Qur’ani haitakuwa tu sauti masikioni mwetu, bali nguvu katika mienendo, maamuzi na muundo wa maisha yetu; ili mwanga wa mbinguni usikike katika jamii, uandaye njia ya mabadiliko, na kuunda jamii yenye uadilifu na roho ya kiroho kwa msingi wa Qur’ani.”
4319600