IQNA

Kikao cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Kuhusu Somalia

11:03 - January 11, 2026
Habari ID: 3481790
IQNA- Kikao cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kilichojadili suala la Somalia na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kulitambua eneo la nchi hiyo la Somaliland, kama nchi huru kimefanyika katika makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Jeddah, Saudi Arabia.

Kikao hicho cha dharura kilihudhuriwa na wawakilishi wa nchi wanachama ili kujadili athari za hatua hiyo, ambayo imeibua upinzani mpana katika ulimwengu wa Kiislamu na kimataifa.

Mjadala huo uliitishwa kufuatia hatua ya utawala wa Kizayuni ya kulitambua eneo la kujitenga kaskazini mwa Somalia linalojiita Somaliland, hatua iliyotajwa na wachambuzi wengi kama yenye kuchochea mgawanyiko na kuhatarisha uthabiti wa eneo hilo.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika mawasiliano ya video na kiongozi wa eneo la Somaliland, Abdulrahman Mohamed Abdullahi, alitambua eneo hilo kama nchi huru na akamwalika kutembelea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Netanyahu alitaja makubaliano hayo kama “fursa muhimu ya kupanua ushirikiano.”

Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni pia ilitoa taarifa ikisema kuwa makubaliano hayo yamefanyika ndani ya mfumo wa Makubaliano ya Abraham yanayopigiwa debe na mtawala wa Marekani Donald Trump. Hapo awali, vyombo vya habari vya utawala huo vilikuwa vimetaja Somaliland kama moja ya maeneo yanayozingatiwa kwa ajili ya kuwahamisha kwa lazima baadhi ya Wapalestina wa Gaza, mjadala uliokosolewa vikali kimataifa.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Ahmed Moalim Fiqi, ameishutumu Israel kwa kupanga kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka katika eneo lililojitenga la Somaliland, akiukashifu mpango huo alioutaja kuwa ni "ukiukaji mkubwa" wa sheria za kimataifa.

Katika mahojiano na Televisheni ya Al Jazeera jana Jumamosi, Fiqi ametoa wito kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu afutulie mbali tangazo lake la kulitambua "eneo lililojitenga" la Somaliland, akiieleza hatua hiyo iliyotangazwa mwishoni mwa mwaka uliopita kuwa "hujuma ya moja kwa moja" dhidi ya mamlaka ya kujitawala Somalia.

Nchi za bara Afrika,  Kiarabu na Kiislamu zinahofia kwamba, uwepo wa Israel katika Pembe ya Afrika kupitia Somaliland ni jambo ambalo litavuruga mlingano wa kiusalama katika Bahari Nyekundu na kugeuza eneo hilo kuwa uwanja wa makabiliano ya moja kwa moja na ya gharama kubwa.

4327969

Kishikizo: somalia israel
captcha