IQNA

Mjadala wa Yemen Kuhusu Njia za Kukabiliana na Udhalilishaji wa Qur’ani

15:54 - January 06, 2026
Habari ID: 3481772
IQNA – Mjadala maalum kuhusu “Wajibu wa Umma wa Kiislamu katika kukabiliana na udhalilishaji wa Qur’ani na matukufu mengine na maadui” umefanyika mjini Sanaa, mji mkuu wa Yemen.

Mjadala huo ulihudhuriwa na wanazuoni, wahubiri na wasomi ambao walichambua changamoto za kiakili na kiitikadi zinazoukabili Umma wa Kiislamu katika mazingira ya kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya Qur’ani na alama za dini.

Allama Shams al-Din Sharaf al-Din, Mufti Mkuu wa Yemen, katika hotuba yake alisisitiza kuwa Umma wa Kiislamu lazima uimarisha mwito wa kumlingania Mwenyezi Mungu na kuimarisha imani ndani ya nyoyo. Aliongeza kuwa mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Qur’ani na Mtume Mtukufu (SAW) ni mwendelezo wa historia ya upotoshaji na uadui ambao Mitume na Wajumbe wa Mwenyezi Mungu wamekumbana nao.

Mufti Mkuu alihimiza mshikamano wa safu na kuondoa misimamo mikali ya kimadhehebu ili kukabiliana na njama za maadui.

Hizam al-Assad, mwanachama wa Baraza la Kisiasa la Ansarullah, pia alihutubia akisema kuwa yanayoendelea Gaza yanaonyesha asili ya mradi wa Kizayuni-KiMagharibi uliolenga Umma na matukufu yake. Aliongeza kuwa kauli za Magharibi kuhusu uhuru wa kujieleza hazina maana kutokana na viwango viwili wanavyotumia katika kushughulikia suala la Palestina na matusi dhidi ya Qur’ani Tukufu.

Arif al-Hajri, mzungumzaji mwingine, alisisitiza wajibu wa wanazuoni na wahubiri katika kulinda Qur’ani Tukufu na akatoa wito wa kususia kiuchumi bidhaa kutoka nchi zinazodhalilisha Uislamu.

Mjadala ulimalizika kwa kusisitiza umuhimu wa kudumisha umoja katika hotuba za kidini, kuamsha nafasi ya wanazuoni katika kukuza uelewa wa kijamii, na kukabiliana na vita laini vinavyolenga utambulisho wa Umma wa Kiislamu na matukufu ya Waislamu.

4327160

Habari zinazohusiana
Kishikizo: yemen qurani tukufu
captcha