Brigedia Jenerali Yahya Saree amezungumzia oparesheni hiyo kwa jina la "Oparesheni ya Disemba Saba" iliyotekelezwa jana Jumatatu na kueleza kuwa tunakabiliwa na ghasia kubwa; na tutatekeleza oparesheni zaidi za kijeshi katika fremu ya kujilinda kwetu kwa mujibu wa sheria katika kujibu kuendelea mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia na mzingiro dhidi ya Yemen.
Meja Jenerali Yahya Saree amesema katika Oparesheni ya Disemba 7 jeshi la Yemen limetumia ndege nane zisizo na rubani aina ya 2K Qasaf na makombora mengi ya balistiki kwa ajili ya kuyalenag maeneo nyeti na muhimu huko Abha, Jizan na Najran.
Msemaji wa jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi wa Yemen jana Jumatatu yaliandika katika ukurasa wa twitter kwamba: vikosi vya ulinzi vya Yemen vimetekeleza oparesheni kubwa na ya kipekee katika ardhi ya Saudia katika kujibu hujuma na mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia na Marekani.
Muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudia siku kadhaa zilizopita ulishadidisha mashambulizi ya anga katika maeneo mbalimbali ya Yemen ikiwemo katika mji mkuu wa nchi hiyo San'aa; na hadi sasa makumi ya raia wameuawa.
Kufuatia uungaji mkono wa Marekani, Imarati, utawala haramu wa Israel na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu, Saudi Arabia iliivamia kijeshi nchi masikini ya Yemen mnamo Machi 2015 na kuiwekea mzingiro wa pande zote wa nchi kavu, anga na majini. Lengo la vita hivyo lilikuwa ni kuiondoa madaraknai harakati ya Ansarullah lakini Wasaudi wameshindwa kufikia lengo hilo. Uvamizi wa kijeshi wa Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.
Hivi karibuni Shirika la Entesaf la Kupigania Haki za Wanawake na Watoto lenye makao yake nchini Yemen, limesema watoto zaidi ya 300 wa Kiyemen wanaaga dunia kila siku kutokana na utapiamlo wa kiwango cha juu, hali ambayo imesababishwa na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.
Hadi hivi sasa uvamizi huo wa Saudia na waitifaki wake umeshasababisha makumi ya maelfu ya Wayemen kuuawa, wengine wengi kujeruhiwa huku mamilioni ya wengine wakiwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.
Katika kujibu jinai hizo za Saudia na waitifaki wake, Jeshi la Yemen likishirikiana na makundi ya wananchi wanaojitolea vitani hutekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi mara kwa mara dhidi ya maeneo ya kijeshi na vituo vya kiuchumi hasa katika sekta ya mafuta ndani ya Saudia na kuusababishia ufalme huo hasara kubwa.