Qari huyu wa Yemen anatoka katika jiji la Sana’a, mji mkuu wa Yemen. Usomaji wake wa Qur'ani Tukufu kwa mtindo wa kipekee Tarteel, ambao hapo awali haukuwa ukifahamika sana kwa Waarabu na Waislamu, sasa unapatikana kwenye mitandao ya kijamii.
Usomaji huo umepelekea Sheikh al-Faqih kupata umaarufu mkubwa hasa kwenye YouTube na Instagram, ambako usomaji wake wa Qur’ani umezidi kuvutia hadhira kubwa kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Sheikh Al-Faqih, ambaye sasa yuko katika umri wa miaka thelathini, alikuza kipaji chake cha usomaji wa Qur'ani tangu utotoni kwa kuiga wasomaji mashuhuri wa Yemen.
Usomaji wake wa Qur'ani ni katika mtindo wa Sana’a, mtindo unaojulikana kwa uzito na hisia za kiroho na ambao ni maarufu sana miongoni mwa wasomaji wa Yemen.
Licha ya changamoto za mtindo huu, Sheikh al-Faqih ana mapenzi na uhusiano wa kina na mtindo huo.
Msomaji huyu wa Qur'ani alikulia katika familia ya wakulima katika eneo la Arhab, kaskazini mwa Sana’a, na kutokana na kutopenda umaaruf, aliepuka kuwa kitovu cha mvuto wa watu.
Yeye ni imam wa Msikiti wa Bilal ibn Rabah katika eneo la makazi la Habrah mjini Sana’a. Kuwa kiongozi wa swala kulimfanya kuanza kushiriki kikamilifu katika jamii yake.
Katika miaka ya hivi karibuni, mmoja wa marafiki wa karibu wa msomaji huyu wa Yemen alishiriki sauti zake za usomaji wa Qur’ani kwenye mitandao ya kijamii, sauti ambazo ni za unyenyekevu, utulivu, na huzuni. Hili lilipelekea usomaji wake katika mtindo wa Sana’a kuenea zaidi.
Baada ya sauti zake kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, moja ya sauti zake kwenye TikTok ilipata zaidi ya watazamaji milioni 18, hali iliyowafanya raia wa Yemen kumuomba arekodi Qur'ani nzima kwa mtindo wake wa kipekee na sauti yake ya kuvutia.
Mmoja wa mashabiki wa al-Faqih alianza kampeni ya kuchangisha fedha kwenye Facebook mwishoni mwa mwaka 2023 ili kusaidia kugharamia kurekodi usomaji wake.
Kutokana na mwamko huo wa raia wa Yemen, msomaji huyu wa Yemen ameanza kusambaza usomaji wa sura mbalimbali za Qur'ani kupitia ukurasa wa YouTube uitwao Al-Faqih.
Ifuatayo ni mojawapo ya qiraa zake ambapo anasoma aya za Surah Qaaf ya Qur'ani Tukufu:
3491459