IQNA

Kukabiliana na maadui wa Uislamu

Yemen yasusia bidhaa nchi za Ulaya zinazohusika na kuvunjia heshima Qur'ani

18:04 - April 02, 2023
Habari ID: 3476802
TEHRAN (IQNA) - Yemen imepiga marufuku kuingia kwa bidhaa zinazozalishwa na nchi za Ulaya ambazo zimewezesha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, ambapo kiongozi wa harakati ya muqawama ya Ansarullah ameitaja hatua wanayochukua kuwa ni "vikwazo vya kiuchumi".

Katika kikao kilichoongozwa na Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen Mahdi al-Mashat siku ya Jumamosi, baraza hilo mjini Sana'a limelaani vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu barani Ulaya.

Baraza hilo "liliagiza Serikali ya Wokovu wa Kitaifa kuzuia kuingia kwa bidhaa kutoka kwa nchi ambazo ziliruhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, na kuandaa utaratibu wa utekelezaji."

Mapema siku ya Ijumaa, kiongozi wa harakati ya muqawama ya Ansarullah ya Yemen Seyed Abdul-Malik al-Houthi alilaani vikali jinai ya kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu barani Ulaya na kusisitiza ulazima wa Waislamu kuchukua msimamo dhidi ya vita dhidi ya Uislamu.

“Mshikamano wetu wa kidini unatuhitaji kuwa na hasira na kuonyesha hasira zetu wanapoanzisha vita na dini yetu,” akasisitiza.

Akizungumzia namna tawala za Magharibi zilivyotupilia mbali dini, al-Houthi alisema kuwa nchi zote  Kiislamu zinapaswa kukabiliana na Wamagharibi wa silaha ya vikwazo vya kiuchumi.

"Sisi, kama Waislamu, tunapaswa kuziwekea vikwazo nchi zote ambazo zimeruhusu kuchomwa kwa Qur'ani Tukufu kwa sababu vikwazo vya kiuchumi vinatosha kuwazuia maadui na kuwalazimisha kuacha kuutukana Uislamu," al-Houthi alisema.

Vitendo vya kuvunjia heshima Uislamu na Qur’ani Tukufu vimekuwa vikiongezeka barani Ulaya.

Nchi kadhaa za Ulaya zimekuwa zikiruhusu vitendo hivyo vya kuchukiza kufanyika katika ardhi zao katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita. Kuvunjiwa heshima Qur'ani kumelaaniwa vikali katika nchi za Kiislamu duniani.

Siku ya Ijumaa mbili zilizopita, wanachama wa kundi la mrengo wa kulia la Denmark, Patrioterne Gar Live, walikusanyika nje ya ubalozi wa Uturuki mjini Copenhagen, wakionyesha mabango ya kuwachukia Waislamu na kuchoma nakala ya Qur’ani pamoja na bendera ya taifa ya Uturuki, huku wakiitangaza moja kwa moja. ukurasa wao wa Facebook.

Uturuki, Iran, Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Morocco na Pakistan zimelaani kitendo hicho kinacholenga kuumiza hisia za mabilioni ya Waislamu duniani kote.

Nchi za Ulaya ambazo zimeshuhudiwa vitendo vya kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu ni pamoja na Denmark, Uholanzi, Sweden, Ufaransa na Norway.

3483017

captcha