Taasisi za Kiislamu za Al-Azhar na Darul Iftaa zimewaonya watu kuhusu kusambaza klipu za usomaji wa Qur'ani ambazo zina muziki, na kusisitiza kuwa ni marufuku kisheria na ni ukiukaji wa utakatifu wa Qur'ani Tukufu.
Kituo cha Al-Azhar cha Kupambana na Misimamo Mikali hivi karibuni kilibainisha kuenea kwa uzushi au jambo jipya liitwalo "Nyimbo za Qur'ani," ambapo aya za Qur'ani husomwa pamoja na muziki wa Magharibi kwa kisingizio cha uvumbuzi katika kuwasilisha visa vya Qur'ani. Klipu hizi zinaripotiwa kuundwa kwa kutumia akili ya mneman yaani Artificial Intelligence-AI-na huanza kusambazwa kupitia akaunti za kijamii zisizojulikana.
Kituo hicho kimesisitiza kwamba Qur'ani Tukufu ni neno la Mwenyezi Mungu na muujiza wake wa milele, na kuisoma kwa muziki ni marufuku kidini.
Aidha taarifa hiyo imefafanua kwamba Hadithi isemayo "Yeyote asiyesoma Qur'ani kwa sauti nzuri hakutoka kwetu" haina maana ya kuimba aya za Qur'ani na anayefanya hivyo anapotosha maanda ya Hadhithi hiyo ambayo kusudio lake ni kuisoma Qur'an kwa sauti nzuri.
Taasisi hiyo imeongeza kuchanganya muziki na Qur'ani ni sehemu ya mashambulizi makubwa zaidi yanayolenga kupotosha Qur'an na Waislamu, kufuatia vitendo kama vile kuchoma moto nakala za Qur'ani na kujaribu kupotosha aya zake.
Halikadhalika Al Azhar imetahadharisha kuwa, kufuata mtindo huo wa Kimagharibi kwa kisingizio cha kurahisisha kuhifadhi Qur'ani ni dharau kwa turathi tajiri za usomaji wa Qur'ani hususan na wasomaji mashuhuri wa Misri.
Taasisi ya Kupambana na Misimamo mikali ya Al-Azhar ililitaka bunge la nchi hiyo kuharamisha matusi kwa dini na kuanzisha sheria mpya zinazodhibiti matumizi ya Akili Mnemba katika kushughulikia maandishi ya kidini na matakatifu ya kidini..
Dar al-Ifta nayo pia alisisitiza kuwa kusambaza klipu hizo ni marufuku kisheria, kwani kunasaidia katika kueneza uwongo na mawazo maovu. Shirika hilo liliwataka Waislamu kuripoti chaneli zinazorusha video hizo, kwani zinaendeleza chuki na kutukana dini.
Darul Iftaa imebainisha kuwa kusoma Qur'ani kwa ala za muziki na kwa sauti ya uimbaji ni marufuku kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.
3489989